Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe
22 Agosti, 2016 amepokea taarifa ya maendeleo ya mradi mkubwa wa ujenzi
wa kiwanda cha kusindika gesi asili (LNG Plant) kinachotarajiwa kujengwa
katika eneo la Likon'go, Mchinga Mkoani Lindi.
Mwakilishi
Mkazi wa Kampuni ya Statoil ya Nchini Norway ambayo ni moja ya Kampuni
zitakazowekeza katika mradi huo Bw. Oystein Michelsen amemueleza Rais
Magufuli kuwa ujenzi wa kiwanda hicho unatarajiwa kugharimu Dola za
Kimarekani Bilioni 30 sawa na zaidi ya Shilingi Trilion 65 za Kitanzania
na kwamba uzalishaji unatarajiwa kuchukua muda wa zaidi ya miaka 40
baada ya kuanza.
Bw.
Oystein Michelsen amebainisha kuwa Serikali ya Norway ina dhamira ya
dhati ya kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa manufaa ya pande zote na
ameomba Serikali ya Tanzania iendelee kutoa ushirikiano ili kufanikisha
ujenzi wa kiwanda hicho.
Kwa
upande wake Rais Magufuli amemuhakikishia Mwakilishi huyo wa kampuni ya
Statoil kuwa Serikali ya Tanzania ipo tayari kuhakikisha mradi
unafanikiwa na ameitaka Wizara ya Nishati na Madini kupitia Shirika la
Maendeleo ya Petroli (TPDC) kushirikiana na wadau kutoka Wizara nyingine
kuharakisha mchakato wa kuanza kwa ujenzi wa kiwanda hicho.
"Nataka
kuona mradi huu unaanza kujengwa, tunachukua muda mrefu mno,
kamilisheni mambo yaliyobaki ili wawekezaji waanze kazi mara moja"
Amesema Rais Magufuli.
Dkt.
Magufuli amesema mradi huo unatarajiwa kuzalisha ajira kwa idadi kubwa
ya watanzania na utaiwezesha serikali kupata mapato kupitia tozo
mbalimbali, na hivyo kutumika kuimaisha huduma za kijamii zikiwemo
elimu, afya, maji na miundombinu.
Pamoja na Statoil kampuni nyingine zinazoshiriki katika uwekezaji wa mradi huu ni Shell, Exxon Mobil, Pavillion na Ophir.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es Salaam
22 Agosti, 2016
EmoticonEmoticon