WAZIRI MKUU AWAONYA WATUMISHI WA SERIKALI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaonya watendaji wa halmashauri nchini kwamba atakayebainika ametumia vibaya fedha za Serikali atang'olewa kazini kwa sababu Serikali ya Awamu ya Tano haina mchezo na mtu.

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumapili, Desemba 20, 2015)  wakati akizungumza na mamia ya wananchi waliofika kumsikiliza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa michezo wa Ilulu uliopo Lindi mjini.

"Natoa onyo kwa watendaji wote wa halmashauri. Fedha ya Serikali itakayotumwa kwenu halafu mtu aifanyie ubadhirifu,  ole wake. Yeyote atakayebainika kuzitumia kwa ubadhirifu fedha hizi tutamng'oa. Wako wasomi wengi huko nje tena wazuri tu, wanasubiri kupata ajira."

"Nataka watumishi wa umma watambue kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inajielekeza kujali wananchi.  Wao wana dhamana ya kuwasilikiliza na kuwahudumia wananchi ili kuhakikisha wanatatua kero zinazowakabili, " alisema huku akishangiliwa na wengine wakisema huyu sasa ni Sokoine wa pili. (Edward Moringe Sokoine alikuwa ni Waziri Mkuu katika Serikali ya Awamu ya Kwanza).

Waziri Mkuu ambaye amewasili Lindi leo, aliwaeleza wakazi hao kwamba amekuja kuwashukuru wazee na wana Lindi kwa dua zao na kuwaahidi kwamba hatawaangusha Rais John Pombe Magufuli na Makamu wake Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumpa dhamana ya kuwatumikia Watanzania katika ngazi ya Uwaziri Mkuu.

Waziri Mkuu pia alimpa kazi Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bw. Jordan Rugimbana ya kuhakikisha anaufufua uwanja huo na kuurudisha kwenye enzi yake ulivyokuwa maarufu katika mikoa yote ya Kusini. "Uwanja huu lazima uboreshwe kwa sababu unanikumbusha mwaka 1984 wakati nachezea timu ya Amri Rangers.  Kulikuwa na ukoka wa nguvu hapa uwanjani. Kwa hiyo timu aliyoiunda Mkuu wa Mkoa itafanya kazi lakini pia iwajumuishe Meya na mbunge wa Lindi Mjini kwa sababu huu uwanja ni mali ya Halmashauri ya Lindi, " alisema.

Akielezea kuhusu mipango ya Serikali kuendeleza sekta ya viwanda, Waziri Mkuu alisema hivi karibuni mkoa huo utapata wawekezaji kwenye sekta ya gesi baada ya kampuni ya BG kutoka Uingereza kupata umiliki wa eneo la Kikwetu ili wajenge mitambo ya kusafisha gesi.

Aliwataka wananchi wa mkoa huo wawekeze kwenye ujenzi wa hoteli na nyumba za kulala wageni ili ifikapo Agosti mwakani, watu wanaokuja kushiriki maonyesho ya NaneNane kitaifa mkoani humo wasipate taabu ya malazi kama ambavyo imekuwa ikitokea huko nyuma.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikabidhiwa zawadi ya shati la asili la Wamwera na Mzee Saidi Issa Hanga katika mkutano wa hadhara aliouhutubia mjini Ruangwa Desemba 20, 2015.
Waziri Mkuu, Kassim Majliwa na Mkewe Mary wakisalimiana na wazee wa Ruangwa kabla ya mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Waziri Mkuu mjini Ruangwa Desemba 20, 2015.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifurahia silaha za asili alizokabidhiwa na wazee wa Ruangwa kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara mjini hapo Desemba 20, 2015.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokea zawadi ya rungu kutoka kwa Mzee Issa Juma Nangalapa ikiwa ni ishashara ya kumtaka awaadhibu wotw wanaokiuka sheria. Alikuwa katika mkutano wa hadhara aliouhutubia mjini Ruangwa Desemba 20, 2015.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifurahia moja kati ya zana na silaha za asili alizokabidhiwa na wazee wa Ruangwa kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara mjini hapo Desemba 20, 2015. 
Waziri Mkuu, Kassim Majliwa akisalimiana na Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Lindi akiwa njiani kwenda kijijini kwake Nandagala wilayani Ruangwa, Desemba 20, 2015.Katikati ni Waziri wa habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo, Nape Nauye.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na wapigakura wake baada ya kuwasili kijijini kwake Nndagala wilayani Ruangwa kwa mapumziko mafupi Desemba 20, 2015. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Previous
Next Post »