MJAMZITO aliyefahamika kwa jina la Rotha Bujiku, amejifungulia bafuni karibu na zahanati ya kijiji baada ya kudaiwa kufukuzwa na wauguzi waliokuwa zamu siku hiyo, kwa maelezo kuwa anajifungua kila mwaka.
Tukio hilo lilitokea wilaya ya Maswa katika mkoa wa Simiyu majira ya
saa 2 asubuhi baada ya mjamzito huyo kufika katika zahanati hiyo kwa
lengo la kupata huduma ya kujifungulia kwa wataalamu.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo lililovuta umati wa watu,
mjamzito huyo alikataliwa kupokewa na muuguzi wa zamu aliyetajwa kwa
jina la Constansia John.
Ilielezwa kuwa muuguzi huyo alikataa kumpokea kwa madai kuwa mjamzito
huyo alishapewa maelekezo tangu awali kuwa anatakiwa akajifungue katika
hospitali ya wilaya ya Maswa kwani amekuwa akizaa watoto kwa mfululizo.
Inaelezwa kwamba, wakati Rotha akiugulia maumivu ya uchungu, muuguzi
huyo alimpigia simu ya mkononi Muuguzi Mkunga wa zahanati hiyo, Leticia
Kachumi kumjulisha hali hiyo na alipofika alitaka mjamzito huyo aondoke
katika eneo hilo na atafute usafiri ili aweze kufika katika hospitali ya
wilaya kama alivyoelekezwa katika siku za nyuma.
“Leticia alipofika hapo zahanati baada ya kupigiwa simu na
Constansia, licha ya kumuona anaendelea kulalamika kutokana na uchungu
alimwamuru aondoke eneo hilo mara moja na atafute usafiri wa kumfikisha
hospitali ya wilaya iliyoko umbali wa kilomita 36, kwani walishamweleza
kuwa amekuwa akizaa mfululizo na hiyo ni mimba ya kumi na moja,” alisema
shuhuda, Kundi Mageni.
Kutokana na hali hiyo, mjamzito huyo alilazimika kuondoka zahanati
hapo bila msaada wowote na baada kufika karibu na nyumba iliyoko na
zahanati hiyo, alikwenda katika bafu la nyumba ya jirani ambalo halina
sakafu na kujifungulia humo na baadaye kusaidiwa na wasamaria wema
waliosikia sauti ya mtoto.
“Kwa kweli huyu mama amejifungulia katika mazingira machafu na
hatarishi kwa afya yake na mtoto aliyemzaa. Kwa kweli hili ni tukio la
kusikitisha. Huwezi kuamini wauuguzi hao ambao ni wanawake kumtendea
mwenzao ukatili wa kiasi hiki,” alisema Pili Kidesela, Diwani wa kata ya
Shishiyu (CCM).
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Jonathan Budenu aliyefika katika
eneo la tukio muda mfupi baada ya kupata taarifa hizo, alisema kitendo
kilichofanywa na wauguzi hao ni kinyume cha maadili ya kazi yao na hivyo
ni lazima hatua kali za kinidhamu zichukuliwe kwa wote waliohusika.
Mwingine ajifungulia kichakani
Wakati hayo yakitokea Maswa, mkoani
Arusha binti mwenye umri wa miaka 17 alijikuta akijifungulia kichakani
baada ya kuzidiwa uchungu wakati akisubiri kuombewa kwenye mkutano wa
dini uliofanyika Viwanja vya Magereza, Kisongo nje kidogo na Jiji la
Arusha.
Anna Ngitoria, mkazi wa Endurimeti, wilayani Arumeru, alikuwa
miongoni mwa mamia ya wakazi wa Arusha, Kilimanjaro na vitongoji vyake
waliokuwa wamekusanyika kwa wingi kwenye uwanja huo wa magereza kwa
ajili ya kile kilichodaiwa kuwa ni maombi yaliyoandaliwa na kituo kimoja
cha redio cha jijini Arusha, Radio Safina.
Kwa kawaida uongozi wa kituo hicho huandaa makongamano ya kila mwezi
kwenye uwanja huo wa Kisongo na kujumuisha mamia ya watu, wengi wao
wakiwa ni wanawake na wasichana ambao hupendelea kuhudhuria maombezi
hayo kwa matarajio tofauti.
Mikusanyiko ya maombi ya ‘Radio Safina’ imekuwa ikikusanya watu wengi
mithili ya ‘Kikombe cha Babu,’ ambacho nacho kilivuma sana miaka mitatu
iliyopita na tukio la msichana huyo kujifungua katika moja ya matukio
hayo kimezua hisia tofauti mjini hapa.
Akizungumza katika hospitali ya Mount Meru ambapo amelazwa kwa sasa,
binti huyo, Anna amekiri kuwa alijifungua kabla ya wakati kwa sababu
alikuwa na ujauzito wa miezi saba tu.
Mtoto wake njiti sasa anahudumiwa katika wodi maalumu iliyopo hospitalini hapo na wauguzi wanasema anaendelea vizuri.
EmoticonEmoticon