Mafuriko Yaikumba Zanzibar, Watu Wawili Wafariki Dunia


Hali ya Mafuriko Visiwani Zanzibar.
Mafuriko Visiwani Zanzibar.
Baadhi ya nyumba zilizokumbwa na Maafuriko Visiwani Zanzibar.
Wananchi wawili wamefariki dunia Visiwani Zanzibar kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha. Watu waliofariki dunia ni Nd. Juma Hamad (25) mkaazi wa Mwanakwerekwe na mtoto mmoja mkazi wa Kinuni anayekisiwa kuwa na miaka 8.
Mafuriko hayo yamesababisha hasara kubwa ikiwemo upotevu mali na mifugo, uharibifu wa miundombinu pamoja na kusababisha vifo vya watu.
Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mhe. Mohamed Aboud Mohamed wakati akitoa taarifa kwa wananchi kuhusiana na athari za mvua hizo katika ukumbi wa Karume House, Mjini Zanzibar amesema kwamba mvua hizo zimesababisha mafuriko katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mjini Magharibi na kupelekea athari kubwa katika maeneo hayo ikiwemo vifo vya watu, uharibifu wa nyumba za makazi na upotevu wa mali na mifugo.
Ameongeza kuwa maiti ya mtoto imeshapatikana na kuzikwa jana Tarehe 3/5/2015 na maiti ya Nd. Juma Hamad bado haijapatikana na juhudi za kumtafuta zinaendelea.
Amefahamisha kuwa maeneo yaliyoathirika zaidi na mvua hizo ni pamoja na Magomeni, Jang’ombe, Nyerere, Sebleni, Sogea, Mwanakwerekwe, Welezo, Kisauni, Tomondo, Mombasa, Kinuni, Mtopepo, Chumbuni, Kwahani, Mpendae, Bububu na Kwaalinato, ambapo maeneo yote hayo yanapatikana ndani ya Mkoa wa Mijini Magharibi.
Katika hatua nyingine amewatahadharisha wananchi kujiepusha na athari zaidi zinazoweza kujitokeza, ikiwemo wazazi kuangalia watoto wao na kuhakikisha hawachezi karibu na maeneo yanayotuama maji, kwa wale wanaoishi mabondeni ni vyema wakahama sehemu hizo
Previous
Next Post »