UTEKELEZWAJI WA ADHABU YA KIFO KWA WATU 10 WALIOHUKUMIWA KUNYONGWA KUTOKANA NA KUHUSIKA NA MAUAJI YA ALBINO WASUBIRI SAINI YA RAIS JAKAYA KIKWETE

https://igcdn-photos-e-a.akamaihd.net/hphotos-ak-xaf1/t51.2885-15/11117140_1607943206114260_62153689_n.jpgUTEKELEZWAJI wa adhabu ya kifo kwa watu
10 waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa,
kutokana na kuhusika katika mauaji ya watu
wenye ulemavu (albino), unasubiri saini ya
Rais Jakaya Kikwete.
Hayo yalibainishwa na Naibu Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame
Silima, wakati akijibu swali la nyongeza la
mbunge wa Lindi Mjini, Salum Barwany
(CUF).
Katika swali lake, Barwany, alitaka kufahamu
ni lini utekelezaji wa hukumu ya kifo kwa
watu 10, waliokwisha hukumiwa adhabu ya
kifo na Mahakama kutokana na kuhusika na
mauaji ya albino, itatekelezwa.
Silima, alisema kwa mujibu wa taratibu za
kisheria, adhabu ya kifo inapotolewa,
utekelezaji wake husubiri saini ya Rais.
“Sijapata taarifa kama hukumu hizi tayari
Rais ameziwekea saini ili zitekelezwe ila
nitafuatilia ili Sheria ichukue mkondo wake,”
alisema.
Katika swali la msingi la mbunge huyo,
alitaka kufahamu hadi sasa kuna kesi ngapi
za mauaji ya walemavu wa ngozi
zilizokwishatolewa hukumu baada ya
kufikishwa mahakamani na kesi ngapi bado
zinasubiri huku na ni kwanini zimechelewa
kutolewa maamuzi.
Waziri alisema kati ya mwaka 2006 na 2015,
jumla ya matukio 56 ya uhalifu dhidi ya
watu wenye ulemavu wa ngozi yaliripotiwa
nchini na kati ya matukio hayo 41
yalihusisha vifo 43, matukio 13 yahusisha
majeruhi na mawili ya kupotea watu hao
albino.
Alisema kesi 46 kati ya matukio 56
zilifikishwa mahakamani na kesi 10 zenye
watuhumiwa 12 zilitolewa hukumu ya kifo
na kesi 10 badi ziko chini ya upelelezi.
Aidha kesi 26 watuhumiwa wake waliachiwa
huru kwa kukosa ushahidi.
Silima alisema pia kesi 10 bado zinaendelea
kusikilizwa mahakamani na ziko katika
hatua mbalimbali.
“Kuhusu kuchelewa kwa hukumu au
upelelezi wa baadhi ya kesi, kunachangiwa
na sababu mbalimbali kama vile matokeo ya
uchunguzi wa vinasaba (DNA) kutoka
mamlaka za uchunguzi na mashahidi
kutopatikana kwa urahisi na wakati".
Katika swali la nyongeza la mbunge wa Viti
Maalum, Al- Shamaar Kwegyir (CCM), alitaka
kujua Serikali imefikia wapi katika kumtafuta
mtoto Pendo Emmanuel mwenye ulemavu
wa ngozi mkazi wa Kwimba, aliyechukuliwa
mikononi mwa mama yake mzazi na mpaka
sasa hajulikani alipo.
Previous
Next Post »