Faida zinazoweza
kupatikana kwenye nanasi ni nyingi ambazo zinaweza kuwa kama kinga na tiba kwa
baadhi ya matatizo ya kiafya ambayo pengine yangehitaji mtu kwenda hospitali
kupatiwa dawa, tena kwa gharama kubwa.
Miongoni mwa faida hizo ni hizi
zifuatazo:
USAGAJI WA CHAKULA Nanasi lina virutubisho vinavyouwezesha mfumo wa
usagaji chakula tumboni kufanya kazi yake ipasavyo, pindi mfumo huu
unapowezeshwa kufanyakazi yake vizuri, mtu huweza kupata choo laini na kwa
wakati kama inavyotakiwa.
Hivyo wenye kula tunda hili kwa wingi hawawezi
kusumbuliwa na tatizo la ukosefu wa choo. Aidha, kwa mujibu wa tafiti nyingine,
nanasi pia lina virutubisho vyenye uwezo wa kupunguza au kuzuia uvimbe tumboni.
KINGA YA MWILI Nanasi linaaminika kuwa miongoni mwa matunda yenye chanzo kizuri
cha vitamin C ambayo kazi yake mwilini ni kuupa mwili kinga dhidi ya ‘wavamizi’
mbalimbali (freee radicals), ambao wanapoingia mwilini kazi yao hua ni kuharibu
chembechembe hai za mwili.
Vile vile ‘wavamizi’ hao wanapoweka makazi mwilini,
huziba mishipa ya damu na hivyo kusababisha magonjwa ya moyo na mengine mengi,
ikiwemo kansa ya tumbo. Kwa kuongezea, vitamini C inaaminika kuwa na uwezo
mkubwa wa kuimarisha mfumo wa kinga ya mwili, hivyo kuifanya kuwa kinga ya
magonjwa madogo madogo kama vile mafua, kikohozi, homa na maambukizi mengine.
Unapokuwa na kiwango cha kutosha cha vitamin hiyo, bila shaka kinga yako ya
mwili itakuwa imeimarika na hivyo utakuwa umejiepusha na maambukizi mbalimbali.
CHANZO CHA MADINI Mbali ya kuwa ni chanzo kizuri cha vitamin C, nanasi pia ni
chanzo kizuri cha madini aina ya ‘manganese’ ambayo yanaaminika kuwa na uwezo
wa kuboresha ufanisi wa vimeng’enyo mbalimbali vya mwili, vikiwemo vya
kuzalisha nishati na kinga ya mwili. Halikadhalika tunda hili lina kiwango cha
kutosha cha vitamin B1 (thiamin).
KUIMARISHA NURU YA MACHO Inawezekana karoti
ikawa ndiyo inayojulikana na watu wengi kuwa na uwezo wa kuimarisha nuru ya
macho, lakini nanasi nalo lina uwezo mkubwa wa kuimarisha nuru ya macho.
Utafiti unaonesha kuwa ulaji wa tunda hili na matunda mengine, kiasi cha milo
mitatu kwa siku, kunaondoa hatari ya kupungua kwa nuru ya macho kwa asilimia 36
kwa watu wazima.
NANASI LILILO BORA Nanasi lililo bora ni lile kubwa na
lililoiva vizuri. Wakati ni kweli kwamba nanasi kubwa lina nyama nyingi kuliko
nanasi dogo, lakini hakuna tofauti ya ubora wa virutubisho kati ya nanasi dogo
na kubwa, ilimradi lisiwe limeoza au lenye michubuko mingi. Hivyo chagua nanasi
lilioiva vizuri na lenye kunukia.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa hivi
karibuni na Chuo Kikuu cha Innsbruck, nchini Austria, unasema kuwa tunda
linapokuwa limeiva zaidi ndivyo ambavyo virutubisho vyake vinapokuwa bora. Kwa
kula nanasi ambalo halijaiva vizuri, huenda ukajikosesha faida zinazopatikana
kwenye tunda hilo kama inavyoelezwa.
Mara baada ya nanasi kumenywa na kukatwa
vipande, linatakiwa kuliwa mara moja, iwapo litahifadhiwa kwenye jokofu kwa
ajili ya kuliwa baadaye, njia sahihi ya kuhifadhi ni kuliweka kwenye chombo
chenye mfuniko (container) ili kuhifadhi virutubisho vyake kwa kipindi hadi cha
siku tano bila kupoteza ubora wake, ikiwa pamoja na ladha.
Mwisho, unapokula
tunda lolote, zingatia usafi. Osha tunda hadi litakate, nawa mikono yako kwa
sabuni au maji moto, kisha shika tunda lako, vinginevyo unaweza kujikuta
unakula tunda na vijidudu vya maradhi ya kuharisha na hata Kipindupindu.
EmoticonEmoticon