MAPACHA WALIOUNGANA MWILI WILAYANI MAKETE MKOANI NJOMBE KUHITIMU KIDATO CHA NNE MWAKA HUU


Hatua ya kwanza ya ndoto ya kuzama katika elimu ya mabinti pacha walioungana kiwiliwili, Consolata na Maria Mwakikuti (18) wa Kijiji cha Ikonda wilayani Makete  mkoa mpya wa Njombe, inatarajiwa kutimia Novemba mwaka huu, wakati mabinti hao watakapofanya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne.
Itakumbukwa kwamba walipokuwa wakimaliza elimu ya msingi mwaka 2009 kijijini kwao Ikonda, walikuwa na umri wa miaka 13 na katika ndoto zao kwa pamoja walisema wanataka kuwa wasomi waliobobea katika utaalamu wa kompyuta. Lakini, kwa sasa, wanasema wanatamani kufanya kazi ya Ukatibu Muhtasi.Wanafunzi hao mwaka 2010 walichaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Jangwani, Dar es Salaam.
 
Kwa sasa wanasoma katika Shule ya Sekondari ya Maria Consolata iliyopo Kidabaga wilayani Kilolo mkoani Iringa.
Shule hiyo inamilikiwa na Kituo cha Nyota ya Asubuhi ya Wamisionari Wakatoliki wa Italia, kinachosaidia kuwatunza watoto wanaotoka katika mazingira magumu.
 
Wakizungumza na mwandishi wa habari hii shuleni hapo hivi karibuni, walisema wanafurahi kuwa miongoni mwa watahiniwa watakaofanya mtihani huo wa kidato cha nne mwaka huu.
 
"Tunafurahi, tunajiandaa tunasoma kwa bidii, mtihani uko karibu tunataka tufaulu vizuri masomo yetu, ili ile ndoto yetu ya kuwa Makatibu Muhtasi itimie," walisema Maria na Consolata, ambao wanatumia baiskeli maalumu kuwapeleka darasani, ambako pia wana kiti maalumu.
 
Pacha hao wameshangaza watu wengi kwa jinsi walivyo, ambapo kila mmoja ana madaftari yake. Wakati wa kufanya mazoezi au kuandika kazi wanazopewa, mmoja huanza kuandika, akimaliza na mwingine huandika.
 
"Wala hatupati shida tumezoea, kila mmoja anafanya kazi yake, mimi naandika kwa mkono wa kushoto na Maria anaandika kwa mkono wa kulia," anasema Consolata, ambaye anaonekana kuwa mchangamfu zaidi.
Shule hiyo ina wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne. Ilianzishwa mwaka 2006 na hivi sasa ina jumla ya wanafunzi 183. Wote wanaishi kituoni hapo na wote wanatoka kwenye mazingira magumu.
 
Changamoto kubwa iliyokuwa shuleni hapo ni ukosefu wa nishati ya umeme, ambapo uongozi wa shule na kituo hicho unalazimika kutumia jenereta na umemejua, jambo ambalo mapema wiki hii Wakala wa Nishati ya Umeme Vijijini (REA), imewaondolea adha kwa kuwapelekea umeme.
 
Pacha hao walizaliwa mwaka 1996 wakiwa wameungana katika Hospitali ya Ikonda wilayani Makete mkoani Iringa.
 
Walifaulu mtihani wa darasa la saba mwaka 2010, ambapo kila mmoja alipata alama 151, ingawa walitofautiana ufaulu  kwenye masomo yao.
 
Katika somo la Maarifa ya Jamii, Consolata alipata alama 29 na Maria alama 25, kwenye somo la Kiingereza, Maria alipata alama 36 na kumzidi Consolata aliyepata alama 34, wakati kwenye somo la Sayansi, Maria alimzidi Consolata kwa kupata alama 31 dhidi ya 29.
 
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliwapanga pacha hao kujiunga na kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Jangwani jijini Dar es Salaam.
 
Hata hivyo hawakujiunga na sekondari hiyo, kutokana na hali yao na pia umbali kutoka Iringa hadi Dar es Salaam. Ndipo Wamisionari hao wakawachukua mwaka 2011 na kuanza kidato cha kwanza.
 
Walizaliwa kwenye Hospitali ya Misheni ya Ikonda mwaka 1996. Lakini, taarifa zao hazikufahamika hadi pale walipoandikishwa kuanza elimu ya msingi Ikonda na kutafutiwa mlezi wa kuwaangalia, baada ya wazazi wao kufariki dunia wakiwa bado wadogo.
Previous
Next Post »