Marubani wa ndege watakiwa kutoa taarifa endapo watabeba abiria mwenye dalili za Ebola.

Marubani wa ndege nchini wametakiwa kutoa taarifa mapema endapo watabeba abiria anayehisiwa kuwa na dalili za ugonjwa hatari wa ebola ili wanapofika katika viwanja vya ndege waweze kudhibitiwa na wataalam wa afya.
Katibu mkuu wizara ya uchukuzi Dr, Shabani Mwintanga amesema hayo jijini Tanga ikiwa ni sehemu ya mikakati iliyowekwa ya serikali katika kuhakikisha kuwa wagonjwa wa ebola wanadhibitiwa ili wasiweze kuingia nchini hasa katika mikoa ambayo inapakana na nchi jirani.
 
Dr,Mwintanga amewataka watendaji wa kiwanja cha ndege mkoani Tanga kuhakikisha wanadhibiti wageni kutoka nchi jirani ya Kenya na wanapohisi kupokea mgeni mwenye dalili hizo taarifa zitolewe kwa wataalam wa afya kisha apelekwe katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tanga ''Bombo''kwa ajili ya vipimo kabla ya kusafiri.
 
Kwa upande wake meneja wa kiwanja cha ndege mkoani Tanga Bwana Hamis Amiry amesema tayari wameanza kuchukua hadhari ambapo timu ya kamati ya ulinzi na usalama ya kiwanja hicho imeanza utafiti wa afya za wasafiri wanaohisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huo zoezi ambalo wanalifanywa kwa kushirikiana na idara ya afya.
Previous
Next Post »