Faustina Selali,akiwa katika maumivu makali baada ya kushambuliwa na mumewe.
Inasikitisha sana jamani. Faustina Selali, 38, mkazi wa Mgeta, Mvomero mkoani hapa, yupo kwenye mateso makali akijiuguza kutokana na kipigo alichopata kutoka kwa mumewe wa ndoa aliyemtaja kwa jina la Lugasiani John Miasiku, kisa kikiwa ni mumewe huyo kutaka kuoa mke wa pili.
Mwanamke huyo amelazwa katika wodi nambi 3 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, ambapo amesimulia kisa chote mbele ya kamera ya Uwazi.
KISA CHENYEWE
Akizungumza kwa tabu, Faustina alisema tukio hilo lililobadilisha historia ya maisha yake na kumwachia machungu moyoni mwake, lilitokea Juni 25, mwaka huu majira ya saa nne usiku ndani ya nyumba yao.
“Mimi na mume wangu tumeishi kwenye ndoa kwa muda wa miaka 20 na kufanikiwa kupata watoto watano. Kwa kipindi kirefu nilihisi ana uhusiano wa kimapenzi na mwanamke mwingine, wakati naendelea kumchunguza, mume wangu akaniambia anataka kuoa mke wa pili,” alisema Faustina kwa uchungu na kuongeza:“Nikamhoji mume wangu, dini yetu hairuhusu jambo hilo na zaidi ya yote anachotafuta kwa huyo mke wa pili ni kitu gani wakati tayari mimi nimeshamzalia watoto watano na bado naendelea kuzaa?
“Hakuwa na jibu la maana, akaendelea kushikilia msimamo wake. Mwisho nikaona nisimlazimishe sana, nikamwambia kama hivyo ndivyo basi tugawane mali ili mimi niondoke aje huyo mwenzangu kwani sitakuwa tayari kuishi maisha ya uke wenza. Kwa kweli hakuwa na jibu la maana.”
Akionyesha sehemu ya jeraha.
HARUFU YA KIFO
“Ugomvi huo ulitokea Jumanne, kesho yake yaani Jumatano (siku ya tukio) mume wangu alivyorudi shamba nilimtengea ugali kama kawaida. Alikula vizuri tu... tukapanda kitandani kulala, kama unavyojua tena wanandoa muda wao wa kuzungumza kwa utulivu ni usiku, nikaamua kuutumia muda huo kumwuliza mwenzangu.
“Nikamwambia kama bado ana msimamo wake uleule, anipe sehemu yangu niondoke zangu. Hapo nikawa nimechokoza moto. Ilikuwa ghafla tu, aliamka kitandani na kuchukua nyundo kisha akaileta kichwani na kunipiga nayo, baadaye akanipiga mdomoni na kuning’oa meno mawili ya mbele kwa kutumia ile nyundo.
“Hakuishia hapo, akanitoa panga kisha akanicharanga mikono yote, palepale damu zikaruka kama kachinja ng’ombe. Nilihisi maumivu makali sana, sikuwahi kupata maumivu makali kama yale. Kusema ukweli nilichanganyikiwa kabisa na kile kipigo.”
ATUMIA UJANJA KUJIOKOA
“Wakati akiendelea kunipiga bila huruma, alikuwa akisema dawa yangu mimi ni kufa ili aweze kumchukua huyo mwanamke wake bila usumbufu. Nilivyosikia hivyo ikabidi nitumie akili; nikajiangusha chini na kujifanya nimekata kauli ili nisiendelee kuumia.
“Alipoona hivyo kweli akaniacha. Akavaa nguo zake na kukimbia. Mwanangu mdogo Nesto akanisaidia kunikongoja hadi kwa jirani yetu Mzee Chota ambaye naye aliita majirani haraka, ilikuwa ni saa sita usiku, wakanikimbiza hadi Zahanati ya Mlali lakini nikapewa rufaa ya kuletwa hapa kutokana na hali yangu kuwa mbaya.”
Kwa mujibu wa Bi. Faustina, licha ya mume wake kumfanyia ukatili huo, ndugu wanaofika hospitalini hapo kumjulia hali, wanasema mumewe bado hajakamatwa na amekuwa akiendelea kutoa vitisho dhidi yake.
Uwazi lilifunga safari hadi kijijini Mgeta kwa lengo la kuhojiana na mtuhumiwa huyo na kufanikiwa kumkuta lakini alipomuona mwandishi wetu, Miasiku alitimua mbio akidhani alifuatwa na askari.
EmoticonEmoticon