KARANI WA MAHAKAMA ADAIWA KUUAWA NA HOUSIGELI WAKE KWA KUCHOMWA KISU




Karani wa Mahakama ya Wilaya ya Singida, Asha Juma(24), anadaiwa kuawa kwa kuchomwa kisu na mfanyakazi wake wa ndani. 
 
Tukio hilo limetokea jana saa 4:00 asubuhi eneo la Sabasaba katika kata ya Utemini mjini Singida.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela alisema mauti yalimfika karani huyo mara baada ya kuchomwa kisu sehemu ya titi la kulia na mfanyakazi huyo wa ndani aitwaye Valetina Kerenge(17).
 
Msichana huyo ambaye ni mwenyeji wa mkoani Mwanza wilayani Ukerewe,  inasadikiwa alilifanya tukio hilo wakiwa ndani na baada ya hapo alipata kiwewe na kukimbilia nje ya nyumba aliyokuwa akikaa na kwenda kwa majirani kuomba msaada.
 
Inasemekana wakati juhudi za majirani za kunusuru uhai wake zikifanyika ili kumuwahisha hospitali kwa matibabu, ghafla marehemu huyo alianguka chini na kufariki papo hapo.
 
“Imesikitisha maana chanzo halisi hakijajulikana, maana msichana huyu alipoona mambo siyo alikimbia,” alisema Kamanda Kamwela.
 
Kamanda alisema tayari msako mkali wa polisi ulifanikisha kumpata majira ya saa 8 mchana akiwa katika harakati za kutoroka maeneo ya uwanja wa ndege.
 
Mwili wa marehemu ulipelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Singida kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi, na baada ya kuchunguza ndugu wa marehemu watakabidhiwa kwa taratibu za kuusafirisha mwili huo kuelekea mkoani Shinyanga kwa mazishi.
 
Jeshi la polisi linamshikilia msichana huyo kwa ajili ya mahojiano.
Previous
Next Post »