Jeshi laonya matumizi mabaya ya simu za mikononi na mitandao ya kijamii


meja+komba
 Msemaji wa Jeshi la Wananchi Tanzania(JWTZ), Luteni Kanali Erick Komba.
Na Mwandishi wetu.
Jeshi la Kujenga Taifa(JKT) limetoa onyo kwa vijana na watanzania kwa ujumla kutokana na matumizi mabaya ya simu za mikononi na mitandao ya kijamii, hasa kwa taarifa zinazohusu Jeshi.
Hatua hiyo imekuja baada ya mtu/watu wasiojulikana kusambaza taarifa za uongo kuhusu vijana kwa mujibu wa sheria wanaoendelea na mafunzo katika makambi mbalimbali ya JKT wanakufa kwa ukatili.
Akikanusha taarifa hizo mbele ya waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa Jeshi la Wananchi Tanzania(JWTZ) Luteni Kanali Erick Komba alisema umma ufahamu kuwa taarifa hizo sio za kweli, ni upotoshaji wa vijana na watanzania.
“Ukweli ni kwamba JKT linasikitika kupoteza kijana mmoja wa kike aitwaye Honorata Oiso aliyefariki katika kikosi cha JKT Oljoro Arusha kwa ugonjwa wa upungufu wa damu(Anaemia) uliosababishwa na maralia kali na sio vijana watatu kama inavyoelezwa kwenye ujumbe unaosambazwa, wazazi wa kijana huyo pia walithibitisha kuwa kijana wao alikuwa na upungufu wa damu,” alisema
Aidha alisema JKT linalaani kitendo hicho na linafuatilia ili kubaini chanzo chake na mtu yeyote atakayebainika kuwa ndiye chanzo cha ujumbe huo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Kwa upande wa Ofisa Habari wa JKT, Meja Emmanuel Muruga alisema kwasasa Jeshi hilo lina jumla ya vijana 38,634 wanaoendelea na mafunzo katika makambi ya Jeshi, ambapo kwa mujibu wa Sheria wapo wavulana 12822 na wasichana 5446 na wakujitolea wavulana 15509 na wasichana 4859.
Aliongeza kuwa kwa mwaka huu vijana wa kwa mujibu wa Sheria walioingia mafunzoni mwezi wa 6 watarejea mwezi wa 9 na kuingia wengine, kwa upande wa wakujitolea wanatajia kuingia mwakani mwezi wa 1 au 2.
Previous
Next Post »