Baada ya Hospitali ya IMTU, Serikali tena yakifungia chuo cha afya



Siku moja baada ya Serikali kuifungia kwa muda usiojulikana Hospitali ya Chuo cha Kimataifa cha Matibabu na Teknolojia (IMTU), kinachohusishwa na utupaji wa viungo vya binadamu mithili ya takataka, Serikali mkoani Rukwa nayo imekifungia chuo cha Rukwa College of Health and Allied Sciences.

Moja ya sababu ya kukifungia chuo hicho ni kutokuwa na kibali cha Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii huku mitaala ya kozi zake ikiwa haipo, kwa maana ya kupitwa na wakati.

Kutokana na kasoro hizo, Serikali ya mkoa kupitia Idara yake ya Afya imezuia wanafunzi wa chuo hicho kufanya mazoezi ya vitendo katika Hospitali ya Mkoa na nyingine mkoani hapa.

Chuo hicho kinachomilikiwa na Umoja wa Kuendeleza Wanawake Mkoani Rukwa (RWAA) ambacho kipo Kanondo, nje kidogo ya Mji wa Sumbawanga, kwa sasa wanafunzi wake wa
mwaka wa mwisho wako katika maandalizi ya mitihani yao ya kuhitimu masomo. Mitihani hiyo inatarajia kuanzia Agosti 25, mwaka huu.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk John Gurisha amelithibitishia gazeti hili juu ya uamuzi huo wa serikali ya mkoa kwa kile alichosema chuo hicho kinaendeshwa kinyemela, ikiwa ni kinyume cha utaratibu kwani hata mitaala ya kozi zinazofundishwa haipo katika mfumo wa masomo Tanzania, hivyo si rahisi kupata viwango vya ubora wa wanafunzi.

Akifafanua, Dk Gurisha alisema usajili wa muda uliotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa (NACTE) haukipi chuo hicho uhalali wa kutoa mafunzo ya tiba, bali kinatoa ruhusa ya kufungua chuo ili kiweze kutoa kozi za tiba.

Alisema baada ya kupata usajili huo, chuo kilitakiwa kupata kibali kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na si vinginevyo.

Aliongeza kuwa chuo hicho hakifuati mitaala ya Wizara ya Afya kwa kuwa kozi ya wahudumu wa afya inayotolewa chuoni hapo ilishasitishwa na wizara husika.

“Awali kabla Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kusitisha kozi ya wahudumu wa afya ilikuwa ikitolewa katika Hospitali za Rufaa za Mikoa pekee kwa mantiki hii kozi zinazofundishwa chuoni hapo ni batili, pia hakina baraka za Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya ambaye ndiye pekee mwenye mamlaka ya kutoa vibali vinavyowezesha vyuo vya afya kufundisha kozi mbalimbali.

“Hivyo chuo hiki akitambuliwi, nimezuia pia wanafunzi wa chuo hicho kufanya mazoezi ya vitendo katika hospitali hii ya mkoa na zinginezo zilizopo mkoani hapa; sasa kutokana na hili chuo hicho kinawapeleka wanafunzi wake Mpanda mkoani Katavi kwa mafunzo ya mazoezi kwa vitendo... Niwe wazi wanaosoma katika chuo hicho wanajipotezea muda wao,“ alisema.

Aliongeza kuwa atahakikisha chuo hicho kinafuata utaratibu ili kiweze kutambuliwa na kwamba haogopi licha ya kauli kali zinazomshutumu kuwa yeye (Dk Gurisha) anakipiga vita kwa kuwa si mzawa wa mkoa huo.

“Huwezi kuchezea maisha na afya za watu kwa sura ya uzawa …kwanza kama kweli kingekuwa ni halali ilikuwa ni jambo jema kwetu kwa kuwa baadhi ya wahitimu wake wangeweza kuajiriwa hospitalini hapa na kwingineko ili kupunguza upungufu wa wahudumu wa afya wenye ujuzi,“ anaeleza.

Naye Katibu wa Hospitali ya Mkoa wa Rukwa, Dorice Nzingilwa anasema wanafunzi wa chuo hicho wanasoma kwa miezi mitatu kisha wanapelekwa kufanya mazoezi ya vitendo na kuanza kuwatibu wagonjwa, jambo ambalo linahatarisha maisha ya wagonjwa.

Aidha alisema hata walimu wanaofundisha katika chuo hicho hawana sifa kwa kuwa baadhi yao ni matabibu wasaidizi.

Kwa mujibu wa barua ya Agosti 20, 2013 iliyosainiwa na Dk Gurisha kwenda kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii yenye kumbukumbu namba GHS /T 40/15/4, licha ya kuainisha mapungufu lukuki yanachokikabili chuo hicho pia kimebainisha kuwa kinaendeshwa kinyume cha utaratibu kwa vile hata mitaala ya kozi zinazofundishwa haipo.

“Hivyo si rahisi kupata viwango na ubora wa wanafunzi,“ inaeleza sehemu ya barua hiyo.

Pia imebainisha kuwa Kaimu Mkuu wa Chuo hicho ni Ofisa Tabibu mstaafu na wengine watatu ambao ni walimu wa kudumu ni wauguzi wastaafu huku mwingine cheo chake pia makazi yake halali hayafahamiki. 
 
Pia kwa mujibu wa barua hiyo walimu wa muda ambao ni watano hawafai kufundisha kwani mmoja wao ni muuguzi mstaafu, wengine tabibu wasaidizi watatu na daktari mmoja kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa.

“Timu ya usimamizi wa huduma za afya Mkoa RHMT na ile ya wilaya CHMT tunapendekeza Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iwe inafanya ukaguzi wa vyuo vinavyotaka kuanzishwa kabla ya NACTE ili wajiridhishe; na wakati wa kufanya ukaguzi washirikishe timu ya mkoa na wilaya ili kuondoa au kuepuka migongano isiyo ya lazima kati ya Wizara ya Afya na NACTE wataarifiwe kwa ajili ya kukamilisha usajili. Aidha NACTE wafahamishwe kwamba wanapotoa usajili msimamizi mkuu na mtoa mitaala ni Wizara husika...

“Na ukaguzi wanaoufanya NACTE uzingatie vigezo vilivyopo kwani hatutegemei kama RukwaCollege of Health Sciences wangepewa namba ya usajili kwa hali tuliyoikuta wakati wa ziara yetu,” inaeleza sehemu ya barua hiyo.

Akizungumzia hayo, Mwenyekiti wa Asasi hiyo ya RWAA inayomikili chuo hicho, Annastela Malaji anasititiza kuwa chuo hicho ni halali kwa kuwa kimepata usajili wa muda kutoka NACTE uliotolewa Januari 31,2014 na kitakoma Januari 30, 2015 ambapo kilishaanza kuchukua wanafunzi tangu mwaka jana.
“Tuko kihalali isitoshe tuna usajili wa Nacte kama kweli tungekuwa hatuna uhalali mbona Agosti 25 mwaka huu wanafunzi watafanya mitihani yao ya kuhitimu tena wataifanyi katika hospitali ya mkoa kwa maelekezo ya Wizara husika …. Lipo jambo hapa,”  alisema Malaji.

Katika hatua nyingine, Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), kimepongeza uamuzi wa Serikali wa kuifungia Hospitali ya Chuo cha Kimataifa cha Matibabu na Teknolojia (IMTU) na kuiomba kufanya ukaguzi kwa hospitali nyingine nchini za serikali na binafsi.

Hayo yamesema na Rais wa MAT, Dk Primus Saidia aliyeongeza kuwa, hatua ya serikali inalinda watu wake na kuhakikisha watoa huduma wanakuwa na sifa stahili, huku wakitoa huduma bora.

Alisema kutokana na taaluma ya afya kuingiliwa na matatizo mbalimbali, ikiwemo kuwepo kwa watoa huduma wasio na sifa huku wengine wakiwa hawana vifa vya kutosha hivyo ukaguzi uendele na hospitali nyingine.

“Tunaipongeza serikali kwa hatua hii ya kumlinda mlaji, lakini tunawasihi isiwe kwa IMTU pekee kwani kuna hospitali za binafsi na za serikali zenye matatizo kama ya IMTU na zinatakiwa kuchukuliwa hatua,”  alisema Dk Saidia. 

Alisisitiza kuwa pia inatakiwa kuzingatia hospitali zote zinakuwa na namna ya kutupa na kuteketeza taka za hospitalini kwa ajili ya kulinda afya za wananchi wake kwani uchafu kama damu au mabomba yaliyotumika yana madhara mbalimbali.

Rais huyo wa MAT, aliwataka wananchi wanaopatiwa huduma zisizoridhisha katika hospitali na vituo mbalimbali vya afya nchini kupeleka malalamiko yao ili hatua ziweze kuchukuliwa, jambo litakalosaidia kuleta mabadiliko kwenye sekta hiyo muhimu.
Previous
Next Post »