MATUMIZI YA VIPODOZI- WANAUME HATARINI KUOTA MATITI NA WANAWAKE KUOTA NDEVU


IDARA ya Afya ya Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa imeonya wakazi wake wanaotumia vipodozi vilivyotengenezwa na viambata vyenye sumu aina ya ‘Steroids’.

Vipodozi hivyo tayari vimepigwa marufuku nchini na wanaovitumia wapo katika hatari ya kuota ndevu kwa wanawake ambapo wanaume wanaweza kuota matiti.

Hayo yalibainisha na Mganga Mkuu wa Manispaa ya Sumbawanga, Dk Ally Mussa Makori jana wakati wa kuteketeza kwa moto tani moja ya vyakula na vipodozi kwa pamoja vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh milioni 4.5.

Aliwataka wakazi wote katika Manispaa ya Sumbawanga na kwingineko kuchunguza uhalisia wa bidhaa ikiwa ni pamoja na kusoma maelezo yake kabla ya kuzitumia ili kuepuka kununua bidhaa zilizoisha muda wa matumizi na bidhaa bandia.

Pia aliwaasa wataalamu wa Halmashauri zote mkoani hapa na mikoa mingine nchini kuhakikisha bidhaa zisizokidhi viwango na zilizopigwa marufuku nchini hazitengenezwi wala haziingi nchini.

Uteketezaji huo uliofanyika jana chini ya ulinzi wa Polisi katika eneo la Mbalika nje kidogo ya Mji wa Sumbawanga kwa ushirikiano baina ya Mamlaka ya Chakula na Dwa nchini (TFDA)Kanda za Juu Kusini na Idara ya Afya Manispaa ya Sumbawanga.

Katika uteketezaji huo, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Sumbawanga , Dk Makori aliwakilishwa na Ofisa Afya wa Manispaa hiyo, Ally Lubeba ambapo alieleza kuwa bidhaa hizo za vyakula vilivyoisha muda wa matumizi na vipodozi vilivyopigwa marufuku nchini vilikamatwa katika Manispaa ya Sumbawanga vikiuzwa madukani.

chanzo http://www.habarileo.co.tz
Previous
Next Post »