DUU AJINYONGA KWA KUKOSA KODI YA CHUMBA

Marehemu Geofrey Ndibalema (41), mkazi wa Tandika jijini Dar aliyejinyonga kwa kukosa kodi ya chumba.

Marehemu Geofrey Ndibalema (wa pili kulia) enzi za uhai wake.
INASIKITISHA! Geofrey Ndibalema (41), mkazi wa Tandika jijini Dar amedaiwa kujinyonga kwa kukosa kodi ya chumba.
Tukio hilo la kusikitisha limetokea Juni 14, mwaka huu katika nyumba aliyopanga marehemu ambapo ilidaiwa kuwa siku moja kabla ya tukio, baba mwenye nyumba alimpigia simu kumkumbushia akaahidi kulipa siku iliyofuata ambayo ndiyo alikutwa amejinyonga.
Kwa mujibu wa ndugu wa karibu wa marehemu aliyeomba hifadhi ya jina lake, alisema Geofrey aliamka asubuhi akiwa mzima wa afya na kwenda kuchota maji ya kuoga ili aelekee kwenye shughuli zake za upambaji ambapo ilidaiwa kuwa alipewa tenda ya kupamba katika harusi na tayari alishachukua nusu ya malipo.
Ndugu huyo wa marehemu alidai, wakati Geofrey anarudi kuchota maji, alimkuta mwenye nyumba akiwa anamsubiri ili alipe kodi yake jambo lililodaiwa kumpa hofu marehemu na kuingia ndani ya chumba chake na kujinyonga.

“Mwenye nyumba alibaki anasubiri alipwe kodi kwa kuwa alijua Geofrey aliingia chumbani kwake kwa ajili ya kuchukua hela hiyo lakini muda mrefu ulipita bila kutoka nje kiasi cha mwenye nyumba kuanza kupata wasiwasi lakini aliamua kumuacha na kuondoka,” alisema ndugu huyo.
Ndugu huyo alizidi kueleza kuwa, baada ya muda rafiki wa marehemu aitwaye Dickson aliyekuwa akiishi naye chumba kimoja ndiye aliyegundua mwenzake alikuwa amejinyonga.
“Rafiki yake aligonga sana mlango bila mafanikio ndipo alikwenda dirishani na kuendelea kuita bila mafanikio, lakini alipochungulia alimuona Geofrey akiwa ananing’inia ndipo alipotutaarifu tukaja,” alisema ndugu huyo.
Ndugu huyo alisema baada ya taratibu za kipolisi kukamilika, walimsafirisha marehemu mkoani Kagera kwa ajili ya mazishi huku ikielezwa baba mwenye nyumba na wanakamati wa harusi waliompa tenda marehemu wamesamehe madeni yao.
Previous
Next Post »