Mshambuliaji kutoka nyumbani Afrika katika nchi ya Ivory Coast, Didier Drogba hii leo atarejea kwa mara ya kwanza kwenye uwanja wa Stamford Bridge unaomilikiwa na klabu aliyowahi kuitumikia kwa kipindi cha miaka minane Chelsea.
Didier Drogba, atarejea uwanjani hapo akiwa na klabu ya Galatasaray ya nchini Uturuki ambayo anaitumikia kwa sasa huku lengo lake likiwa ni moja tu, kuisaidia klabu hiyo kusonga mbele kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.
Tayari meneja wa klabu ya Chelsea Jose Mourinho amewataka mashabiki wa Chelsea kumpa heshima mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 36 kutokana na mazuiri aliyoyafanya klabuni hapo.
Mourinho amesema litakua jambo la kipuuzi kwa mashabiki wa Chelsea endapo watashindwa kumthamini Drogba usiku wa hii leo, kwani kwa kipindi alichokaa huko Magharibi kwa London aliwafurahisha kwa kufanya vyema na hadi kuwapa taji la ubingwa wa barani Ulaya.
Kwa upande wa Didier Drogba amesema pamoja na kupata nafasi ya kuheshimika kwenye klabu ya Chelsea kutokana na mazuri aliyoyafanya kwenye klabu hiyo, hii leo hana budi kutumia uweledi wa soka, kutokana na kuwajibika sehemu tofauti na ile ya The Blues.
Drogba amesema ni kweli kuna mihemko ambayo huenda ikajitokeza kama ilivyokua katika mchezo wa kwanza ambao ulicheza nchini Uturuki majuma mawili yaliyopita ambapo alikutana na wachezaji aliocheza nao kwenye klabu ya Chelsea na pia aliwaona mashabiki wa The Blues, ila suala la kuwajibika katika timu pinzani lilikua pale pale.
Kama itakumbukwa vyema katika mchezo wa kwanza ambao uliunguruma Türk Telekom Arena nchini Uturuki Chelsea walilazimishwa sare na wenyeji wao baada ya kufungana bao moja kwa moja.
Mchezo mwingine wa ligi ya mabingwa barani Ulaya unaounguruma hii leo utakua kati ya Real Madrid ambao watakua nyumbani wakipapatuana na Schalke Nuefier kwenye uwanja wa Stantiago Bernabeu.
Katika mchezo wa kwanza ambao ulichezwa nchini Ujerumani, Schalke Nuefier walikubali kipondo cha mabao sita kwa moja.
EmoticonEmoticon