LUGHA ya Kichina imeanza kufundishwa rasmi Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM), lengo likiwa ni kuwasaidia wanafunzi na wafanyabiashara
wanaosafiri kwenda China.
Naibu Makamu Mkuu wa
UDSM, Profesa Yunus Mgaya, alieleza hayo jijini Dar es Salaam jana alipozungumza
na waandishi wa habari kuhusu ufundishwaji wa lugha hiyo ambayo wameanza
kufundisha kozi fupi kwa sasa lakini kwa siku zijazo watafundisha digrii.
“Kichina kitawasaidia
wafanyabiashara wanaotoka nchini kwenda China kwenye shughuli za kibiashara
pamoja na wanafunzi wa Kitanzania wanaopata ufadhili kwenda kusoma huko,”
alisema.
Aliongeza kuwa
ufundishaji wa somo hilo pia utasaidia katika soko la utalii kwa kuwa
kuna ongezeko la watalii kutoka China.
Profesa Mgaya alisema
UDSM kwa kushirikiana na serikali ya watu wa China wameanzisha kituo cha
kufundisha lugha hiyo na utamaduni wa Kichina.
“Januari mwaka huu
UDSM iliingia katika makubaliano na Chuo Kikuu kilichoko China; tumekubaliana
nao kwa pamoja kuendesha kitengo cha kufundishia lugha ya Kichina,” alisema.
EmoticonEmoticon