Samaki wabovu waielemea Serikali





Afya za baadhi ya Watanzania ambao ni walaji wa kitoweo aina ya samaki zimeendelea kuwa hatarini kutokana na kuwapo kwa dalili kwamba Serikali imeshindwa kudhibiti uwepo wa samaki wabovu katika soko la ndani, wanaoingizwa kutoka nje ya nchi.

Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi pamoja na taasisi nyingine zinazohusika na udhibiti wa viwango na ubora wa samaki, kwa nyakati tofauti wametoa taarifa ambazo hazionyeshi hatua wanazochukua kudhibiti samaki hao, huku kukiwa na uthibitisho wa kuwapo kwa samaki wabovu katika baadhi ya kampuni zinazofanya biashara hiyo.
Itakumbukwa gazeti hili katika toleo la Jumamosi, Septemba 28, liliandika kuwapo kwa samaki hao sokoni, wakiuzwa kwa wingi na kwa bei ya chini katika Soko Kuu la Kimataifa la Feri, Dar es Salaam, lakini taarifa hiyo ilikanushwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Waingizaji wa Samaki Tanzania, Barnabas Mapunda kupitia baadhi ya magazeti ya kila siku.
Mapunda huku akitetea vyombo vya Serikali vinavyohusika na ukaguzi, alisema: “Napenda kuchukua fursa hii kukanusha taarifa hiyo (Samaki hatari waingizwa nchini) na kuufahamisha umma wa Watanzania si kweli kuwa samaki wanaoingizwa kutoka nje ya nchi hawakidhi ubora na usalama kwa matumizi ya binadamu.”
Hata hivyo, siku chache baadaye Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), ilikamata kilo 7,500 za samaki aina ya vibua walioharibika ambao waliingizwa nchini Julai mwaka huu na Kampuni ya Sais Boutique kutoka China.
Kadhalika maelezo ya Mapunda yanatofautiana na kile ambacho gazeti hili limekibaini ndani ya Kampuni ya Alpha Krust Ltd ya Dar es Salaam ambayo taarifa zake za ndani zinathibitisha kuwapo kwa samaki walioingizwa nchini ambao hawafai kwa matumizi ya binadamu.
Uchunguzi ulibaini kuwa samaki hao (Frozen Pacific Mackerel W/R (Scomber Japonicus) waliingizwa nchini Agosti 29, 2013 kutoka Korea Kusini na Kampuni ya Wookyung Co. Ltd: 1851 Jangheung –don, Nam-gu ya jijini Pohang na waliagizwa na Kampuni ya Alphakrust Ltd ya Dar es Salaam.
Taarifa zaidi zinaonyesha kuwa mzigo huo ulibebwa na Kampuni ya Mediterranean Shipping (T) Ltd. Taarifa zaidi zinaonyesha kuwa samaki hao walizalishwa Juni 4, 2013 na tarehe ya mwisho kutumika ilitakiwa kuwa Juni 3, 2014. Hata hivyo, chanzo cha kuaminika katika kampuni hiyo kimebainisha kuwa tarehe hizo hazina uhalisia kwani samaki hao walikuwa wameshaharibika na kuwa hizo ‘sticker’ huwa wanabandika tu, lakini ukweli ni kwamba samaki wanakuja wakiwa wameshaharibika ndiyo maana huwa wanauzwa kwa bei ya chini, kilibainisha chanzo hicho na kuongeza:
“Kuna samaki walioharibika wa aina mbili, kwanza kuna walioathiriwa na mionzi na kuna wale waliokaa muda mrefu. Hawa waliopo ni waliokaa muda mrefu na ukitaka kuwajua hao samaki, watoe katika barafu na kuwaloweka, utaona wanapasuka na ukitia kidole wanabonyea. Athari yake kubwa ni ugonjwa wa saratani ya matumbo,” kilieleza chanzo chetu.
Katika taarifa ya ukaguzi wa kitengo cha ubora cha kampuni hiyo (Organoleptic Assessment) uliofanyika Septemba 12, 2013 (nakala tumeiona), sampuli nne za samaki zilithibitika kutofaa kabisa kwa matumizi ya binadamu.
Previous
Next Post »