Mtanzania Zinduka...! KILA SIKU MPENZI WA BLOG HII TUTAKULETEA MAKALA TOFAUTI TOFAUTI KARIBU SANA




Mtanzania Zinduka...!
Na: Meshack Maganga-Iringa.
Nimemaliza kusoma kitabu cha ‘Success Principles’ Kilicho andikwa na Jack Canfield, kwenye kitabu hiki nimejifunza kwamba, ukitaka kufanikiwa kwenye mambo yako lazima utambue kwamba  wewe ndiye mkurugenzi mtendaji wa maisha yako, mazingira, mifumo, familia na vikwazo vyovyote duniani visiwe sababu ya kuutuliza utu wako. Unazo nguvu zaidi ya nguvu zilizo nje yako za kuwa unavyotaka, kulingana na jinsi ulivyojaliwa. Vipo vitu vinavyoweza kukuzuia hata kukumaliza lakini ni uamuzi wako kusimama kidete kwaajili ya maisha yako na kuonyesha nguvu zilizo ndani yako au kukubali kumalizwa bila ubishi wowote. 
 Mwanzoni mwa mwaka huu,  nilibahatika kusoma  makala ya mwandishi maarufu Freddy Macha kwenye gazeti la Mwananchi yenye kichwa ‘Maisha Bongo,Majuu hali moja’. Kwenye makala yake Freddy Macha alilezea waziwazi kwamba wapo baadhi ya vijana wa kibongo ambao huota kwenda kuishi ‘majuu’ bila kujua kwamba huko maisha ni magumu kuliko hata bongo,na kwamba, popote pale unapoishi utawakuta watu wakilalamika na kusema kuwa afadhali kwenda mahali pengine. Kisha akaenda mbali kwakusema kuwa, ukijua na kutambua la kufanya na namna ya kumudu maisha,unaendelea na mapambano,kwa sababu kanuni kuu ya  uhai ni harakati.
Kwenye makala zangu mabalimbali mimi na Albert Sanga, tumekuwa tukiwaelezea watanzania wenzetu juu ya kuwekeza kwenye kilimo cha miti, mboga na matunda na ufugaji wapo walio elewa na wapo wanaolalamika umbali wa masaa mawili kutoka sehemu wanayoishi mpaka mashambani. Na wapo wanaoona kwamba kilimo ni kazi za watu duni, walioshindwa shule, nk. Na wapo ambao wameamua kuwa wanaharakati wa kusifia maisha ya wacheza mpira wa ligi za ulaya na kupoteza muda vijiweni.
Kwenye makala yake, Albert Sanga yenye kichwa WATANZANIA NA ARDHI alisema,  Jambo jingine linalotumaliza watanzania ni kutokuwa na maono ya muda mrefu. Wengi wetu tunataka mambo ya papo kwa papo, hatupendi kuangalia mambo ya vipindi virefu mbele. Mfano mzuri ni katika hili la uwekezaji katika ardhi.
Mtu anaona ni kupoteza fedha kununua shamba leo ambalo pengine linaweza kuja kutumika miaka ishirini huko baadae. Mtu anaona ni kama kupoteza fedha kupanda miti leo ambayo atakuja kuivuna miaka saba ama miaka kumi ijayo.
Wasichokumbuka wengi ni kuwa unachopuuza kufanya leo kwa gharama ndogo miaka ishirini ama kumi ijayo hutakuwa na uwezo wa kukifanya hata kama ukitamani.
Kwa bahati nzuri zaidi, wataalamu wa masuala ya utambuzi na mafanikio na wajasiriamali maarufu hapa Tanzania na kwingineko duniani kama John Gray, Vincent Peale,   Robert Kiyosaki, Donald Trump, Jack Canfield, Anthony Robbins na wengine, wanabainisha vigezo ambavyo vinaweza kumfanya mtu kutabiri kama maisha yake yatakuwa ni ya kushindwa hadi mwisho au yatakuwa ni ya mafanikio.
Mwana mama Rhonda Byrne kwenye kitabu chake cha ‘The Secret’ ameeleza kwamba, kama mtu akiwa anaamini kwamba kuna watu wengine wa aina fulani mahali fulani, ambao ndio peke yao wanaoweza kufanikiwa na kufika juu kwenye ngazi ya kimapato, mtu kama huyo hawezi kamwe maishani mwake kuja kutoka kwenye lindi la umaskini.
Rhonda, ambae aliishi maisha ya hali ya chini nayakutisha,anafafanua kwamba, mtu akiwa na mtazamo huo, hawezi kutoka kwenye lindi hilo kwa sababu juhudi zake ambazo zingemfikisha mbali zinakuwa tayari zimewekewa mipaka na imani hiyo, kwamba yeye hahusiki  katika kufanikiwa, bali kuna wengine ambao ni Mungu mwenyewe  anayewajua na aliyewateua. Kwa kufikiri hivo, juhudi yake kubwa  katika kutafuta itakuwa ni ile ya kumfanya asife tu kwa njaa na siyo kuvuka hapo. Kama ujuavyo, tunapoamini kuhusu jambo Fulani, mawazo yetu hutusaidia kulifikia jambo hilo.
Kuna mwandishi wa kitabu cha Jitambue enzi zile 2006 nikiwa bado mwanafunzi wa sekondari aliwahi kuandika kwamba, ‘Hata kama “fuko la fedha” litadondoshwa miguu mwetu tutalipiga teke na kuliambia “mimi sikuandikiwa kupata bwana, kuna wenyewe, hali kama hii hujitokeza mara nyingi sana maishani mwetu.”
 Tunakabidhiwa dhamana kubwa ambayo ingetusaidia sana maishani mwetu, lakini tunacheza nayo hadi inapotea kwa sababu tu hatuamini kwamba utunastahili kuitumia kufika juu. Tunaziona nafasi za kusonga mbele, lakini tunaamini kwamba, hatustahili kuzitumia.
Fursa zikija waziwazi kabisa, tunajifanya hatuzioni kwa kutafuta visingizio mbalimbali ili tusizitumie, kwa sababu tu, tumeamini kwenye mawazo yetu kwamba, sisi hatustahili.
Ni vigumu kugundua kwamba nafasi au fursa hizo zimekuja kwa sababu tayari tumejifungia njia kuelekea mafanikio. Wengine kwa bahati mbaya wanaweza kuona na kubaki wameshangaa ni kwa nini tushindwa kuinuka katika mazingira tuliyomo.
Mtu anapoamini kwama hawezi, anayaambia mawazo yake ya kina yamsaidie kumfanya ashindwe zaidi kwenye kila jaribio analofanya. Badala ya kufanya juhudi kujisaidia ili amudu, hujipweteka kwa kuamini kwake kwamba hata kama atafanya kitu gani, kamwe hatamudu. Siyo rahisi kwa mtu mwenye mawazo ya aina hii kuweza kufanikiwa maishani.
Kuna watu ambao kwa sababu ya kukosa kile ambacho jamii inakiona kuwa ndiyo ufunguo wa mafanikio, huwa wanaamini kwamba hawawezi kufanikiwa au kufanya vizuri maishani kama hao ambao wanacho. Kwa mfano, kwa kukosa elimu, ujuzi au utaalamu fulani, watu wengine hujihesabu kama wanyonge. Huchukulia kwamba ni wale tu wenye elimu, ujuzi na utaalamu fulani ndiyo wanaoweza au wanaotakiwa kufanikiwa.

Bila shaka umeshawahi kusikia au hata wewe mwenyewe kusema, “Si wamesoma bwana’ ndiyo wanaojaliwa, sisi ambao hatuna elimu kazi yetu itakuwa ni kuwatumikia. Kauli kama hizi zina chimbuko lake mbali sana, pengine katika malezi yetu. Wazazi kwalizoea au wamezoea kuwaambia watoto wao, “Usiposoma kazi yako itakuwa ni kuwabebea wenzako mizigo, unafikiri pesa inaokotwa, nk.  Kwa bahati mbaya mtoto aliyelishwa “sumu” (‘EARLY CHILD PROGRAMMING’) hii anaposhindwa shule, huamini kwamba yeye atabaki kuwatumikia wengine tu.
Tunapoamini kwamba kwa sababu hatuna elimu ya kutosha na pengine ujuzi au utaalamu fulani, hatuwezi kufika juu kwenye mafanikio, tutakuwa tunatafuta kufulia( ama vifafa vya kiuchumi). Moja ya vigezo muhumu vinavyoweza  kutufikisha kwenye mafanikio ni kuamini kwetu kwamba tunaweza kufika huko. Tunapokuwa hatuna imani kwamba tunaweza kufika huko hujifungia njia wenyewe.
Baadhi yetu kuwa tunaamini kwamba tuna mikosi, balaa au nuksi napengine laana ambazo zinatuzuia katika kufikia malengo yetu. Tunaamini hivyo kiasi kwamba hata tukifikia karibu kabisa na mafanikio huwa tunajiambia ni kazi bure, tutaporomoka tu. Na kweli kwa kuamini hivyo hujikuta tukiporomoka kila tukifika karibu na kufanikwa au kufikia malengo. 
Kinachotokea ni kwamba, kwa kuamini kwetu kuwa tunamkosi, balaa, laana au nuksi, huwa tunatenda kwa mkabala huo wa kinuksi au kibalaa na kimkosi, ambapo matokeo yake ni kujikwamisha. Watalaamu wa elimu ya mafanikio wanaeleza kwamba tunapoamini kuwa tuna mkosi au nuksi huwa tunayashauri mawazo yetu ya kina kutusaidia kuendelea kuwa katika hali hizo (Niliwahi kufafanua zana hii nilipoandika makala ya BINADAMU NI ZAIDI YA MWILI WAKE). Ndiyo maana siyo rahisi  kukuta mtu anayeamini katika nuksi akiondoka katika hali hiyo.
Tufanyeje basi, kama ni kweli kimapato tuko hoi napengine tunachoweza ni kupata riziki yetu ya kila siku tu? Pamoja na kwamba mengi yameelezwa  tayari kwenye mada nyingine, bado tunaweza kukuambia, tunachotakiwa kufanya ni kujenga imani ya kumudu. Kamwe hatutakiwi kabisa kujiambia tulipofikia ndipo basi, hatuwezi kupanda zaidi.

Yupo mjasiliamali fulani,ni dada mpambanaji (Elizabeth Samoja) kwenye ujasiriamali alipata kuandika hivi, maisha ya kijana wa kitanzania aliyechagua kuishi Dar es salaam baada ya kumaliza masomo yake ya chuo kikuu huwa hayaelewiki,(ingawa kwa mtazamo wake yanaeleweka) utashangaa kijana huyu anapomaliza chuo anaanza zungusha cv ndani ya bahasha ya kaki,mtaa kwa mtaa,jingo kwa jingo,atapata kazi kampuni ya simu,au bank,au kampuni ya bia, atapanga chumba mitaa ya  sinza, wengine huchukua mkopo  na nunua gari aina ya  vitis,corora,corona, opa, ama gari lolote lisilozidi milioni  kumi, ataoa amakuolewa,atafanya shopping Mr Price, mjanja mwingine atakopa hela za kwendea ‘sendoff’ na wengi wao wakijitahidi hununua mariedo, atavaatai kubwa na kuonekana smart, ataenda club, kuponda raha...

Ukiungalia mlolongo huu vizuri,shughuri nyingi hapo kati zote zinachukua pesa mfukoni mwa ila chanzo cha pato lako ni kimoja tu(ajira), kwa kifupi wewe ni mtumiaji tu....kutoboa kimaisha kwa kufuata mpango huu ngumu sana................

Imefika hatua mpaka mabenki wamejua watanzania si entrepreneurs na investors wanapenda magari ya bei chee,na akijitahidi basi apate nyumba bunju,mbagala,au kitunda.....ndo maana mikopo mingi ya benki wanatangaza kwa kuonyesha nyumba ama gari....maana huko ndo kwenye urahisi na kuna soko na wateja wakubwa maarufu kama ‘victim society’ market. Mtanzania Zinduka......

Usiseme hakuna pesa, pesa zipo nyingi sana, fursa za kumwaga, nina mshangaa huyu mhitimu wa chuo kikuu akiwa mtaani asijue cha kufanya badala yake anaingia kwenye mitandao ya kijamii kama ‘Face
book na kuanza kumwaga lawama kibao,jiulize umefanya nini,kwani ulikuja duniani ili ubebwe na serikali? Kwa sasa Tupo watanzania milioni 44 wote tukisubiri kubebwa tutakuwa taifa la aina gani hili?
meshackmaganga@gmail.com  0767 48 66 36/ 0713 48 66 36.
Previous
Next Post »