Julius Nyaisanga afariki dunia






Marehemu Julius Nyaisangah (katikati) akiwa katika pozi na Meneja Mkuu wa Global Publishers Abdallah Mrisho (kushoto) na Mhariri Msaidizi wa Gazeti la Uwazi Elvan Stambul (kulia) walipokuwa katika semina ya wanahabari Bagamoyo mwaka 2011.

MWANDISHI wa Habari wa siku nyingi, Julius Nyaisanga (53), maarufu kama Anko J, amefariki dunia. Nyaisanga amefariki dunia jana mjini Morogoro, katika Hospitali ya Mazimbu, alikokuwa akipatiwa matibabu. Taarifa zinasema, Nyaisanga ambaye enzi za uhai wake alijipatia umaarufu kutokana na uwezo wake mkubwa aliokuwa nao katika utangazaji wa redio na televisheni, alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari uliomsumbua kwa muda mrefu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Meneja Matangazo wa Kituo cha Abood Media ambako Nyaisanga alikuwa akifanya kazi, Abed Dogoli, alisema Nyaisanga alijiunga na kituo cha Abood Media mwaka 2010 na kupewa wadhifa wa meneja wa kituo hicho.

Kwa mujibu wa Dogoli, moja ya majukumu ya Nyaisanga yalikuwa ni kusimamia upande wa redio na televisheni inayomilikiwa na Abood Media.

Alisema taratibu za mazishi zinafanyika nyumbani kwa marehemu, Kihonda eneo la Carmel na mwili wake unatarajia kusafirishwa kwenda nyumbani kwao mkoani Mara kwa ajili ya mazishi.

Enzi za uhai wake, Nyaisanga aliwahi kuwa mtangazaji wa Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD), ambayo sasa inaitwa TBC Taifa na Redio One. Aliwahi pia kuwa mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani (Deutsche Welle).

Naye mke wa marehemu, Leah Nyaisanga, alisema mumewe alizidiwa juzi jioni na kupelekwa katika Hospitali ya Mazimbu kabla ya kufariki jana saa moja asubuhi.

Alisema marehemu ameacha mke mmoja na watoto watatu aliowataja kuwa ni Samuel, Noela na Beatrice.

Akizungumzia kifo hicho, Mbunge wa Morogoro Mjini, Aziz Abood, ambaye familia yake ndiyo inayomiliki Kituo cha Abood Media, alisema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha mtangazaji huyo.

Alisema kuwa, alimfahamu Nyaisanga miaka mingi iliyopita, kutokana na uwezo wake mkubwa wa kutangaza aliokuwa nao.

Naye, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa Morogoro, Idda Mushi, alisema marehemu Nyaisanga alikuwa mchapa kazi na mfano wa kuigwa katika taaluma ya uandishi wa habari.

Alisema marehemu atakumbukwa kwa mengi aliyoyafanya katika taaluma ya uandishi wa habari, kwa kuwa alikuwa na uwezo mkubwa katika utangazaji na uandaaji wa vipindi mbalimbali.
Previous
Next Post »