
Shirika la haki za binaadamu la Human
Rights Watch limechapisha ripoti inayoelezea mazingira magumu
wanayokumbana nayo watoto wanaojiingiza kwenye ajira ya uchimbaji madini
nchini Tanzania, wengi wao wakiathirika kiafya.
Ikiwa na kichwa cha habari kisemacho
"Ajira ya Watoto katika Migodi", ripoti hiyo imefichua vitendo vya
dhuluma na ukatili wanaokutana nao watoto wao ambao baadhi yao wako
hatarini kuangukia kwenye matatizo ya kiafya ikiwemo mtindio wa ubungo
kutokana na kemikali zinazokutikana kwenye machimbo hayo.
Ripoti hiyo iliyotangazwa leo jijini
Dar es salaam inafuatia utafiti uliofanyika katika maeneo ya machimbo
ambako watoto wengi wameajiriwa.
Maafisa wa Human Rights Watch wamesema
kuwa pamoja na kutumika katika kazi ngumu ya utafutaji madini, lakini
baadhi ya watoto hao wanalazimika kutumika katika biashara za kingono na
kukubwa na matukio ya unyanyasaji wa kijinsia.
Ripoti hiyo ambayo pia imeangazia
athari zitokanazo na matumizi ya madini ya zebaki kwenye machimbo hayo,
imesema kuwa baadhi ya kampuni binafsi na vikundi vya watu huwatumia
watoto hao kusaka madini jambo ambalo linakwenda kinyume na sheria za
kimataifa.
Akiwasilisha ripoti hiyo, Mtafiti mkuu
wa Human Watch, Jenina Morna, alisema kuwa idadi kubwa ya watoto hao
hufanya kazi kwenye mazingira magumu na wakati mwingine hulazimika
kuingia kwenye mapango yaliyoko chini kwa chini kwa ajili ya kusaka
madini.
"Watoto hufanya kazi katika migodi
yenye kina kirefu mno, watoto hawa husafirisha mizigo mizito ya dhahabu,
na wakati mwingine hutumia vifaa hararishi kusaka madini kama vile
mawe." Alisema Morna.
Moja ya sababu kubwa inayowasuma
watoto wengi kuingia kwenye migodi ni hali ya kipato duni iliyopo kwenye
familia nyingi, kama inavyothibitika katika makala fupi iliyoandaliwa
na Human Watch ikionyesha kina mama na watoto wakihangaika na maisha.
Kwa sasa Tanzania ni nchi ya tatu
barani Afrika kwa kuzalisha kwa wingi madini ya dhahabu, ikizidiwa na
nchi za Afrika ya Kusini na Ghana.
Mwandishi: George Njogopa/DW Dar es Salaam
Mhariri: Josephat Charo
EmoticonEmoticon