Waziri wa Mashauri ya nchi za kigeni
wa Marekani, John Kerry ameshtumu anachokitaja kama hatua ya serikali
kutumia silaha za kemikali dhidi ya watu wake kama ukosefu wamaadili wa
hali ya juu.
Amesema kanda za video za silaha zinazotuhumiwa kuwa za kemikali karibu na mji wa Damascus ni kweli na zisizoweza kukanushwa.
Kerry aliongezea kwamba Rais Barack Obama anatafakari hatua ya kuchukua.
Haya yanajiri saa chache baada ya wakaguzi wa silaha za kemikali wa Umoja wa Mataifa kushambuliwa karibu na mji mkuu huo.
Wachunguzi wa silaha za Umoja wa
mataifa kuwasili katika eneo lililopo viungani mwa mji mkuu Damascus
ambapo inashukiwa kuwa wiki iliyopita kulishambuliwa kwa silaha za
kemikali .
Wanaharakati wa upinzani nchini Syria
wanasema wachunguzi hao wa Umoja wa mataifa wanakutana na waathiriwa wa
shambulio linaloshukiwa kuwa ni la gesi ya sumu na madaktari waliowatibu
.
Wachunguzi hao watachunguza mabaki na kukusanya sampuli za udongo, damu na tishu kwa ajili ya vipimo vya maabara. .
Awali watu wasiojulikana wenye silaha
waliushambulia kwa risasi msafara wa magari waliokuwemo wakaguzi hao
walipokuwa wakielekea kwenye eneo la tukio - na kuwalazimisha kurejea
nyuma kwa muda .
Vyombo vya habari vya kitaifa nchini viliwashutumu waasi kufanya shambulio hilo.
Rais Assad aliwaruhusu wakaguzi wa
silaha baada ya kukabiliwa na shinikizo kubwa la kimataifa, lakini
Marekani na Uingereza zimesema ushahidi mwingi huenda uliharibiwa katika
muda wa siku tano, tangu kutokea kwa mashambulio.
Wakati huo huo serikali za magharibi
zimeikosoa Syria kwa kuchukua muda mrefu kuruhusu timu ya Umoja wa
mataifa ya wakaguzi wa silaha kuzuru eneo linalodaiwa kushambuliwa kwa
silaha za kemikali na zinaangalia uwezekano kuingilia kati kijeshi
nchini humo.
EmoticonEmoticon