Madawa ya Kulevya
Dar es Salaam. Kasi ya kukamatwa kwa Watanzania wakiwa wamebeba
dawa za kulevya nje ya nchi, imezidi kuchukua sura mpya baada ya
kubainika kuwa maelfu ya Watanzania wanatumikia vifungo mbalimbali
ikiwamo vifungo vya maisha nje ya nchi.
China pekee mpaka sasa ina Watanzania 176
wanaotumikia vifungo katika magereza za nchi hiyo, huku asilimia 99
wakiwa wamekamatwa na dawa za kulevya.
Kutokana na kuwapo ongezeko hilo la wafungwa wa
dawa za kulevya, China imekataa ombi la Tanzania la kubadilishana
wafungwa, ikieleza hatua hiyo itachochea watu wengine kujiingiza kwenye
uuzaji wa dawa za kulevya nchini humo.Hatua hiyo imekuja baada ya nchi
hizo mbili kutofautiana katika mfumo wa sheria, ambapo China mtu
anayekamatwa
na dawa hizo hunyongwa hadi kufa wakati Tanzania mtu anayekutwa na dawa hizo anahukumiwa kifungo.
Akizungumza na Mwananchi Jumamosi, Msemaji wa
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mkumbwa Ally
alisema: “Takwimu halisi tulizonazo kutoka China pekee zinaeleza kuwa
Watanzania 176 wanatumikia vifungo na asilimia 99 ni kwa tuhuma za dawa
za kulevya. Kawaida nchi hiyo adhabu yake ni kifo lakini kesi nyingi
bado zipo katika uchunguzi ambao huchukua miaka miwili.”
Hata hivyo alisema kutokana na uhusiano mzuri wa
nchi hizi mbili, kuna uwezekano mkubwa kwa Watanzania hao kufungwa
kifungo cha maisha pamoja na faini.
Aidha, alisema juhudi za Tanzania kuwasiliana na
China kuhusu uwezekano wa kuwa na mikataba ya kubadilishana wafungwa
ziligonga mwamba, baada ya nchi hiyo kukataa ombi hilo kutokana na idadi
kubwa ya wafungwa hao kutuhumiwa na dawa za kulevya.
“China imekataa kuwa na mkataba wa kubadilishana
wafungwa kwani wanahofu kuwa inaweza ikachochea biashara hivyo. Hivyo
kinachofanyika ni kuwatembelea wafungwa hao mara kwa mara na kuhakikisha
wanapata haki zao na kuwasaidia mawasiliano wao na ndugu zao
wanapotumikia vifungo vyao nchini humo.”
Wakati hayo yakibainika, Jumanne wiki hii Tanzania
ilisaini mkataba wa kubadilishana wafungwa na Thailand, mkataba ambao
utawafanya Watanzania waliofungwa nchini humo kuomba kutumikia vifungo
vyao nchini.
Hata hivyo, takwimu zilizotolewa na Tume ya
Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini, zinaeleza kuwa zaidi ya
Watanzania 103 wamekamatwa nchini Brazil kwa tuhuma za kukutwa na dawa
za kulevya, huku 132 wakikamatwa katika nchi nyinginezo.
Hata hivyo, taarifa zaidi kutoka katika tume hiyo
zinadai kuwa hiyo si takwimu halisi ya Watanzania wanaoshikiliwa nje ya
nchi, bali imetokana na nchi hizo kutoa taarifa kuhusu Watanzania hao,
kwani bado idadi kubwa ya Watanzania wanakamatwa lakini taarifa zao
hazijaweza kuifikia tume.
Akizungumza na Mwananchi Jumamosi jana Kamanda wa
Polisi Kikosi Maalumu cha Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Godfrey
Nzowa alisema tatizo la dawa za kulevya linazidi kuwa kubwa kutokana na
ongezeko kubwa la idadi ya wasafirishaji na watumiaji hapa nchini.
Source:MWANANCHI
EmoticonEmoticon