Aliyekuwa rais wa Afrika Kusini Thabo Mbeki atabiri kuwa mzee Mandela atarudi nyumbani hivi karibuni.

MADIBA

Rais wa zamani wa Afrika kusini Thabo Mbeki amesema mtangulizi wake Mzee Nelson Mandela, huenda akatoka hospitali na kuendelea na matibabu nyumbani. 

Mbeki amesema hayo wakati akizungumza katika  hafla moja ya Chama cha Afriacan National Congress-ANC.

Mandela  amelazwa hospitali kwa  wiki tano sasa kutokana na maambukizi  ya mapafu, hali iliosababisha kumiminika kwa risala za kumuombea nafuu kutoka ndani ya Afrika Kusini na kimataifa.

Marafiki waliomtembelea wamesema Mandela bado  anapumua kwa msaada wa mashine.

Shujaa huyo wa vita dhidi ya sera ya ubaguzi wa rangi, alitumikia kifungo cha miaka 27 gerezani, kabla ya kuwa Rais wa kwanza  wa Afrika kusini ya Kidemokrasia mwaka 1994. 

Thabo Mbeki aliyekuwa makamu wake wa Rais, alishika wadhifa huo wa kuiongoza Afrika kusini  wakati Mandela alipostaafu mwaka 1999.

Ifikapo siku ya Alhamisi wiki hii Mandela atatimia umri wa miaka 95.

Previous
Next Post »