Tanzania yatia saini mradi wa umeme wa mabilioni ya fedha.

 

download (6)

 The Deputy Permanent Secretary in the Ministry of Finance Dr. Servacius Likwelile and Sumitomo Corporation Senior Official signs a Memorandum of Understanding(MOU) for Kinyerezi 240 MW combined cycle power project at SUMITOMO Corporation Headquarters in Tokyo this morning. Witnessing the signing ceremony is President Dr.Jakaya Mrisho Kikwete and SUMITOMO Corporation President and CEO Mr.Kuniharu Nakamura.

download (7)

Tanzania imetiliana mkataba wa ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme wa mabilioni ya fedha na Kampuni ya Sumitomo Corporation ya Japan ikiwa ni moja ya miradi ya kwanza na mikubwa kutekelezwa chini ya Ushirikiano wa Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).

 Sherehe za utiaji saini huo zimefanyika jana, Ijumaa, Mei 31, 2013 mjini Tokyo, Japan na kushuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ambaye anatembelea Japan.

 Katika sherehe hizo zilizofanyika kwenye Makao Makuu ya Sumitomo Corporation yenye ghorofa 39, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Servacius Likwelile ametia saini kwa niaba ya Serikali ya Tanzania wakati Ofisa Mtendaji wa Kampuni Sumitomo Bwana Msayuki Hyodo ametia saini kwa niaba ya kampuni hiyo, moja ya makampuni makubwa zaidi katika Japan. 

Kwa upande wa Sumitomo Corporation, Rais na Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo, Bwana Kanuharu Nakamura ameshuhudia utiaji saini mkataba huo ambako kituo cha kuzalisha megawati 240 zitajengwa katika eneo la Kinyerezi mjini Dar es Salaam kwa gharama ya sh. bilioni 675.

 Katika mradi huo mkubwa, Sumitomo Corporation inashirikiana na makampuni mengine ya Japan ambayo ni pamoja na Benki ya Maendeleo ya Japan (JBIC), Kampuni ya Bima ya Nippon (NEXI) na Benki ya Sumitomo Mitsui Banking Corporation (SMBC), moja ya makampuni tanzu ya Sumitomo.

 Akizungumza katika sherehe hiyo, Rais Kikwete ameishukuru Kampuni ya Sumitomo kwa kuonyesha imani yake kwa Tanzania kwa kuwekeza katika uchumi wake.

Pia ameeleza jinsi gani Sumitomo ilivyochangia katika kuokoa maisha ya Waafrika kwa kuwekeza katika Kiwanda cha Kutengeneza Nguo za A-Z mjini Arusha ambako mpaka sasa vyandarua milioni 30 vimetengenezwa na kusambazwa katika Afrika nzima.

 Kwenye sherehe hiyo pia Rais Kikwete ameshuhudia utiaji saini wa Makubaliano ya Ushirikiano kati ya Sumitomo Corporation na Kampuni binafsi ya Tanzania, Quality Garage Limited.

 Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Quality Garage, Bwana Yusuf Manji ametia saini kwa niaba ya kampuni yake wakati Meneja Mkuu wa Mikakati ya Kimataifa na Uratibu, Bwana Takechiyo Tanaka ametia saini kwa niaba ya Sumitomo.

 Sumitomo imekuwa inafanya biashara kwa miaka 400 tokea ilipoanzishwa katika miaka 1600 kabla ya kuundwa rasmi kwa Sumitomo Corporation mwaka 1919 na katika Afrika ina ofisi na shughuli katika Tanzania, Afrika Kusini, Angola, Kenya, Madagascar na Ghana.

 Wakati huo huo, Rais amekutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Kampuni ya Biashara ya Marubeni, kampuni nyingine kubwa ya Japan. Ujumbe wa Marubeni katika mazungumzo hayo kwenye Hoteli ya Intercontinental mjini Yokohama umeongozwa na Bwana Akihiko Sagara, Mtendaji wa Kampuni hiyo.

 Marubeni ambayo ilianzishwa mwaka 1858 inafanya biashara ya kiasi cha dola za Marekani bilioni 112 kwa mwaka ikiwa na mali zenye thamani ya dola bilioni 63 na faida ya bilioni 2.2 kwa mwaka. Ina ofisi 120 nje ya Japan katika nchi 65.

Rais ambaye yuko Japan katika ziara ya kikazi ya siku saba ni mmoja wa viongozi wengi za Afrika ambako wamealikwa kuhudhuria Mkutano wa Tano wa Tokyo Kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD – V) unaoanza leo kwenye Hoteli ya Intercontinental mjini Yokohama.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,

DAR ES SALAAM.

31 Mei, 2013

Previous
Next Post »