Vijana wenzangu na wote wenye dhamira ya
kuwezesha maendeleo ya vijana nchini, salaam!
Mtakumbuka kwamba mwezi Januari 2013 nilitoa
taarifa kwa umma ya kueleza kuwa niliwasilisha kwa Katibu wa Bunge Muswada
Binafsi wa Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa na kuomba hatua za ziada toka
ofisi ya Bunge kwa kuzingatia Kanuni ya 21 na Kanuni ya 81 ya Kanuni za Kudumu
za Bunge.
Toka wakati huo muswada huo mpaka sasa Mei 2013
haujachapwa katika gazeti la Serikali na nimepokea barua toka kwa ofisi ya Bunge
kwamba wamepokea ushauri toka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa muswada huo
hauwezi kuchapishwa katika gazeti la Serikali kwa kuwa umekiuka masharti ya
ibara ya 99 ya Katiba ya Nchi.
Sababu ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoa
ushauri huo ni kuwa muswada unalenga pamoja na mambo mengine kupitia kifungu cha
31 kipengele cha kwanza kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kwa madhumuni ya
kugharamia shughuli za baraza la vijana la taifa, mipango ya baraza na
kutekeleza miradi ya vijana kwa ajili ya maendeleo ya vijana.
Kwa maoni yangu Mwanasheria Mkuu wa Serikali
ametoa ushauri huo bila kuzingatia kwamba kifungu cha 31 kipengele cha pili
kinataja vyanzo mbalimbali vya fedha za mfuko ikiwemo kutaja kuwa fedha za mfuko
zitatokana na fedha zilizotengwa na Serikali na Bunge kwa ajili ya Baraza kwa
mujibu wa Ibara ya 135 kifungu cha pili cha katiba ya Nchi.
Ibara ya 135 (2) ya Katiba ya Nchi inatamka
kuwa “fedha ambazo hazitawekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali ni zile
zote ambazo zimetajwa na sheria ya kwamba zitumike kwa shughuli maalum au
ziwekwe kwenye mfuko mwingine kwa ajili ya matumizi maalum”.
Hivyo, ni maoni yangu kuwa ibara hiyo ya Katiba
ya Nchi inaweza kutumika kuwezesha kuanzishwa kwa Baraza la Vijana na Mfuko wa
Maendeleo ya Vijana bila kufungwa na Ibara ya 99 ya Katiba kifungu cha kwanza
ambacho kimeweka masharti kuwa “Bunge halitashughulikia jambo lolote kati ya
mambo yanayohusika na ibara hii isipokuwa kama Rais amependekeza kwamba jambo
hilo lishughulikiwe na Bunge na pendekezo hilo la Rais liwe limewasilishwa
kwenye Bunge na Rais.”
Kifungu cha pili kinataja mambo yanayohusika na
ibara hiyo ya 99 ni pamoja na muswada wa sheria kwa ajili ya “kuagiza kwamba
malipo au matumizi ya fedha yafanywe kutokana na Mfuko Mkuu wa Hazina ya
Serikali au mfuko mwingine wowote au kubadilisha kiwango hicho kwa namna
nyingine yoyote isipokuwa kupunguza”.
Toka Sera ya zamani ya maendeleo ya vijana ya
mwaka 1996 itamke kwamba Serikali itawezesha kuanzishwa kwa Baraza la Vijana na
suala hilo kurudiwa katika Sera mpya ya mwaka 2007; miaka takribani 17 imepita
marais wote wa awamu husika na mawaziri wenye dhamana hawajawasilisha bungeni
muswada huo hali ambayo imenifanya niandae muswada binafsi kuwezesha baraza
kuundwa.
Muswada wa Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa
2013 niliouwasilisha kwa maoni yangu hauna lengo la kuagiza malipo au matumizi
ya fedha yafanywe kutokana na Mfuko mkuu wa Hazina ya Serikali au Mfuko mwingine
wowote kwa mujibu wa ibara ya 99 bali unalenga kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya
Vijana kwa kuzingatia masharti ya Ibara ya 135.
Hata hivyo, kwa kuwa muswada huu unahusu
mustakabali wa vijana na ni suala la kitaifa kupitia waraka huu naomba kupata
maoni yenu kuhusu suala hili, mapendekezo ya marekebisho yanayohitajika
kufanyika na hatua zinazopaswa kuchukuliwa.
Maoni, mapendekezo na hatua hizo zitumwe
kupitia mbungeubungo@gmail.com au
kwa Afisa wa Ofisi ya Mbunge Ubungo Gaston Garubimbi (0715825025) kabla ya
tarehe 24 Mei 2013.
Nakala ya rasimu ya muswada wa Baraza la
Vijana la Taifa wa mwaka 2013 inapatikana katika mtandao wa http://mnyika.blogspot.com kwa ajili ya
rejea.
Aidha, nawaalika kushiriki mikutano ya kupokea
maoni kupitia mtandao huo tarehe 20 mpaka 23 Mei 2013 saa 9 alasiri mpaka 10
Jioni ambayo nitashiriki na kutoa maelezo ya zaidi kwa kadiri
itakavyohitajika.
Natarajia kupokea maoni ya vijana na wananchi
wengine bila kujali tofauti mbalimbali kwa kuwa madai ya kutaka kuundwe Baraza
la Vijana la Taifa yamekuwa yakitolewa na vijana, asasi na taasisi kwa muda
mrefu.
Vyama vya siasa kwa kuzingatia matakwa hayo
viliahidi kutekeleza azma hiyo kwa mfano Ilani ya CHADEMA ya mwaka 2010-2015
kipengele 6.4.1 (viii) ilitamka “Kwa kuwa vijana ndio kundi kubwa hapa nchini,
na kwa kuwa uhai wa muda mrefu wa taifa letu upo mikononi mwa vijana, Serikali
ya CHADEMA itawezesha vijana kuunda Baraza la Vijana (BAVITA) ambalo
limekwamishwa na Serikali ya CCM kwa muda mrefu”.
Kwa upande mwingine, Ilani ya CCM ya mwaka
2010-2015 iliahidi katika kipengele 80 (k) “Kuhamasisha ushiriki wa vijana
katika ngazi mbalimbali za maamuzi ikiwa ni pamoja na kukamilisha uanzishaji wa
Baraza la Vijana”.
Mwaka 2011 niliihoji Serikali bungeni ni lini
itakamilisha uanzishwaji wa baraza hilo na ikaahidi kwamba kazi hiyo
itakamilishwa katika mwaka wa fedha 2011/2012 hata hivyo sasa ni Mei 2013
Serikali haijakamilisha.
Hivyo vijana, wabunge na wananchi kwa ujumla ni
muhimu kuboresha muswada huo na uwasilishwe bungeni kuwezesha baraza la vijana
na mfuko wa maendeleo vijana kuanzishwa; maslahi ya umma kwanza.
Wenu katika uwakilishi wa wananchi,
John Mnyika (Mb)
19 Mei 2013
Dodoma
EmoticonEmoticon