Jeshi la Marekani likiajiandaa kwa mashambulizi kutoka kwa
Korea Kaskazini
Marekani imepeleka mitambo ya kukinga makombora katika kisiwa
cha Guam katika bahari ya Pacific huku Korea Kaskazini ikitishia kurusha
makombora ya nuklia nchini humo.
Idara ya ulinzi ya nchi hiyo imesema kuwa mitambo hiyo itakuwa tayari katika
kipindi cha wiki kadhaa , na kuongeza kwa zana za kivita ambazo zilipelekwa
katika eneo hilo.
Korea Kaskazini ilitaja kisiwa cha Guam kuwa miongoni mwa maeneo yanayolengwa
kwa mashambulizi ikiwemo Hawaii na Marekani.
Korea Kaskazini haidhaniwi kuwa na teknolojia ya kutosha kushambulia Marekani
kwa zana za nuklia au makombora ya masafa marefu.
Korea Kaskazini inasema kwamba imewaweka wanajeshi wake, tayari kwa shambulio
dhidi ya Marekani ikiwemo kutumia zana za nyukilia.
Taarifa hii imejiri wakati Marekani imeimarisha mitambo yake ya kukinga
makombora katika kisiwa cha Guam kilichoko bahari ya Pacific.
Idara ya ulinzi ya Korea Kaskazini imesema inatoa taarifa kwa Marekani kwamba
jeshi lipo tayari kushambulia bila huruma, kile imetaja kama vitisho vya
Marekani dhidi yake.
Utawala wa Pyongyang ulionekana kukerwa na hatua ya Marekani ya hivi maajuzi
ambapo wanajeshi wake walifanya mafunzo ya pamoja na ambayo yalihusisha utumizi
wa zana za kivita.
Hata hivyo wachanganuzi wamesema Korea Kaskazini haina silaha ambazo zinaweza
kushambulia ardhi ya Marekani, japo katika siku za karibuni imefanya majaribio
ya makombora ua masafa marefu.
Hapo jana Jumatano, Korea Kaskazini iliwazuia wafanyikazi wa Korea Kusini
kuvuka mpaka kuelekea katika viwanda vya pamoja vinavyomilikiwa na nchi mbili,
na hivyo kukatiza uhusiano uliobaki kati yake na Kusini.
Baadhi wanaona malumbano ya sasa kama hatua ya Korea Kaskazini kushinikiza
Marekani kuanzisha mazungumzo ya pamoja ambayo yataafikia mkataba wa amani.
EmoticonEmoticon