PIGO JUU YA PIGO... MDOGO WA WASTARA AUAWA

 


Na Imelda Mtema
NI pigo juu ya pigo kwa staa wa filamu za Kibongo, Wastara Juma ambaye miezi minne iliyopita alifiwa na mumewe, Juma Juma Kiwoloko na sasa amepatwa na msiba mwingine mkubwa.
Msiba huu wa sasa umemfanya Wastara kulazwa jijini Dubai baada ya kupata mshtuko kufuatia mdogo wake wa kiume, Abdulmalik  kupigwa risasi na kufariki dunia jijini Dar.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea usiku wa manane, kuamkia Aprili 11, mwaka huu ndani ya Ukumbi wa Lango la Jiji Magomeni Mikumi wakati Abdulmalik alipokuwa akiamua ugomvi kati ya dada yake aitwaye Hawa na shemeji yake aliyejulikana kwa jina la mzee Lyimo.
Kwa mujibu wa mdogo wa marehemu aitwaye Nuru, marehemu siku ya tukio alikuwa nyumbani kwao Magomeni Mikumi na  ilipotimu saa sita usiku alipigiwa simu na Hawa akimuomba aende kumchukua katika Ukumbi wa Lango la Jiji ili warudi nyumbani.
“Wakiwa katika ukumbi huo, muda mfupi baadaye alitokea mzee Lyimo ambaye ana uhusiano wa kimapenzi na Hawa na kuanza kumvamia na kumpiga mwanamke huyo.”
Nuru alisema kuwa kipigo hicho kiliwashtua watu wengi waliokuwa katika eneo hilo na kumfanya Abdulmalik kuingilia ili kuamua ugomvi huo na kumuokoa dada yake asiendelee kupigwa.
“Baada ya kuona hivyo, mzee Lyimo alichomoa bastola na kupiga hewani kuwatawanya watu, wakati Abdulmalik alipokuwa akiamua risasi moja ikampata tumboni,” alisema Nuru kwa masikitiko.
Nuru alidai kwamba baada ya Abdulmalik kupigwa risasi, alipatwa na kiwewe na kuanza kukimbia hadi nyumbani, kisha akajifungia ndani, baadaye akamwambia kaka yake mwingine kwamba alipigwa risasi ya tumboni na shemeji yao.
Binti huyo aliendelea kusema kwamba wakati ndugu hao wakijadiliana, mzee Lyimo alifika nyumbani hapo na kumchukua Abdulmalik kisha kumpeleka katika Hospitali ya Mikumi. Alipomfikisha, alitoweka na kumuacha kijana huyo hospitali hapo.
“Kwa kweli alikuwa katika hali mbaya, ndugu tukaamua kumpeleka Muhimbili lakini tukiwa njiani, Abdulmalik alifariki dunia,” alisema Nuru na kuanza kulia.
Dada huyo alisema kuwa madaktari wa Hospitali ya Mikumi katika uchunguzi wao walibaini kwamba risasi iliyokuwa imempata Abdulmalik ilikuwa imepanda kutoka tumboni na kufika kifuani.
“Yaani kiukweli kifo cha kaka Abdulmalik kinaumiza, ndugu hawaamini na hatujui hali ya Wastara ambaye amelazwa baada ya kupatwa na mshtuko pale tulipompa habari hizi,” alisema Nuru.
Mwandishi wetu alijaribu kuwasiliana na Wastara kwa njia ya simu, hata hivyo staa huyo alisema kuwa alikuwa katika hali mbaya kutokana na msiba huo na kulazwa kwa mapumziko hivyo asingeweza kuongea vizuri mpaka atakapokuwa sawa.
“Siwezi kwa kweli… naomba niache, nimelazwa kwa mapumziko…” alisema kwa sauti iliyoonesha kwamba alikuwa akilia.Chanzo:www.globalpublishers.info


Previous
Next Post »