WANASIASA wawili vijana ambao wamekuwa katika vita ya maneno na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe, kuhusu madai waliyoyatoa kuwa anawindwa kuuawa, mwishoni mwa wiki iliyopita, walijitokeza katika ofisi za Mtanzania Jumatano na kufunua siri na matukio ya utesaji raia na mauaji ya kinyama ambayo yamekuwa yakitokea kwa nyakati tofauti kwenye shughuli za kisiasa hapa nchini.
Wanasiasa hao, Juliana Shonza na Mtela Mwampamba, ambao wamefanya mahojiano ya ana kwa ana na gazeti hili, walisema madai waliyoyatoa awali kuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willbrod Slaa, alitajwa na kada wa chama hicho, Ben Saanane, kuwa alimtuma amuwekee sumu Zitto kwa lengo la kumuua ni ya kweli kwa sababu walimkamata akiwa nayo na alikiri jambo hilo na kumuomba msamaha Zitto kwa kitendo hicho.
Walidai, mbali na tukio hilo ambalo baada ya kuliibua limegusa hisia za wengi na kuzua mijadala mikali, yapo matukio mengine ya mauaji na majaribio ya kuua, ambayo yamekuwa yakiratibiwa na Chadema kwa lengo la kuwagombanisha wananchi na Serikali.
Shonza na Mwampamba walisema kuwa wapo tayari kutoa ushuhuda wa matukio hayo mahali popote watakapohitajika na walipoulizwa ni kwa nini baada ya kubaini kuwepo kwa vitendo hivyo, hawakutoa taarifa kwa vyombo vya sheria au taasisi za ulinzi na usalama, walisema mlengwa mkuu katika matukio hayo ambayo yalikuwa yakisababisha madhara kwa watu wengine hakuwa tayari siri hiyo kuanikwa.
Akizungumza mbele ya jopo la waandishi wa habari wa gazeti la Mtanzania Jumatano, Shonza alidai kuwa, yeye na baadhi ya vijana wenzake waliokuwa wakiunda kundi Patriotic Movement, walimnasa Saanane akiwa na sumu hiyo katika Hotel ya Lunch Time iliyoko Ubungo, Dar es Salaam, ambao awali alidai kuwa ni dawa ya Panya, lakini alipobanwa alieleza kuwa ilikuwa sumu ambayo hakuitaja jina na kwamba alipewa na Dk. Slaa ili amuwekee Zitto kwa sababu alikuwa akimsumbua sana.
Alisema, sumu ingewekwa kwenye kinywaji cha Zitto akiwa katika kikao hicho, lakini hatua yake ya kutohudhuria ndiyo iliyomuokoa.
Shonza alisema, baada ya Saanane kukiri kuwa alitumwa na Dk. Slaa kumuwekea Zitto sumu, walimtaarifu wakati akiwa Marekani na aliporudi alikutana na kuwataka jambo hilo wasilifikishe polisi kwa sababu lingekivuruga chama na kwamba kwa sababu alikwishawajua wabaya wake atajilinda.
Alimtuhumu Zitto kwa kuficha ukweli na kumwita kiongozi mwoga, huku akimuonya kuwa iwapo ataendelea na tabia ya kukanusha ukweli atamuumbua hadharani kwa sababu anamjua vizuri.
“Ameongea hayo kwa sababu ana tabia ya kushindwa kuthibitisha kuwa ana uwezo wa kujiongoza yeye mwenyewe pamoja na wengine. Mtu wa maslahi Zitto, anatafuta huruma ya Chadema baada ya kuona amepukutika kisiasa kutokana na kukosa msimamo kiuongozi na hawezi tena kutetea wanyonge, ni mtu mwoga.
Mnapokuwa kwenye mapambano yeye yuko tayari kurudi nyuma, lakini huruma hiyo asitegemee kuipata Chadema, labda akubali kushaurika na kubadilika kama kweli anataka kutetea maslahi ya wanyonge,” alisema Shonza.
Aidha, Shonza alimshambulia pia Saanane kwa kudai anakataa ukweli anaojua, kwa sababu tukio la kukamatwa kwake akiwa na sumu lilitokea akiwa mbele ya zaidi ya mtu mmoja na kusisitiza kuwa kada huyo wa Chadema anatumika na viongozi wa juu wa chama hicho kuwashughulikia baadhi ya wanachama wasiotakiwa.
Katika hili, Shonza alidai zaidi kuwa Saanane ni mtu hatari kwa sababu ndiye aliyeanzisha kundi la PM7, ambalo lilikuwa na lengo la kumpindua Mbowe kutoka kwenye wadhfa wake wa uenyekiti, lakini baadaye aliwageuka wenzake na kusababisha kufukuzwa katika chama.
“Saanane alikuwa anatumika kutuingiza mkenge. Alianzisha kile alichokiita mapinduzi, Patriotic Movement (PM7), lengo lilikuwa Pindua Mbowe, sisi hatukujua.
Tulikuwa saba katika PM7, Saanane alifanikiwa kutuchezea akili na alikuja na 'nick names' (majina bandia) yake. Mimi akaniita Benanzir Bhuto, Mchange akaitwa Mdude, Mwampamba- Joseph Kony, Zitto- Dogo kama tulivyozoea kumuita na yeye mwenyewe akajiita Cobra, wapo na wengine sikumbuki vizuri majina yao hapa.
Sisi vijana wakati mwingine tunatumika vibaya, sisi hatukujua ana ajenda yake, tulivyoshtuka akatukana na ndiyo yakatokea hayo yaliyotokea,” anazidi kueleza Shonza.
Mwampamba
Kwa upande wake Mwampamba ambaye aliandamana na Shonza katika ofisi za Mtanzania Jumatano, alidai kushangazwa na hatua ya Zitto kukanusha kauli ya Shonza iliyokuwa ikieleza namna Saanane alivyokamatwa akiwa na sumu aliyokuwa ametumwa kumuwekea Zitto.
Alisisitiza kuwa, Zitto anajua mipango inayopangwa ndani ya Chadema kwa ajili ya kummaliza na alimtaka aache tabia ya kufunika kombe ili mwanaharamu apite, kwa sababu inaweza kuwa na athari mbaya kwake.
“Zitto anajua mpango mzima wa kutaka kumalizwa kwa sumu na Ben Saanane, baada ya kutumwa na Dk. Slaa kwa sababu tulimwambia na alithibitisha mwenyewe pale Saanane alipomuomba msamaha, sisi ndiyo tulimbana Saanane hadi akaeleza ukweli wa mipango yao ya mauaji.
“Leo namshangaa anavyojikomba eti haamini kuwa anaweza kuuawa na hao jamaa. Lakini kwa Ben Saanane, namtaka atambue kuwa Ludovick alipokamatwa alikanwa na Dk. Slaa wakati ndiye alikuwa kijana wake mpenzi, sasa na yeye ipo siku atakimbiwa.
“Zitto anatakiwa aache tabia ya kufunika funika mambo, ajue nimemwokoa sana katika mambo mengi, mfano mauaji ya Morogoro yaliyopangwa na Chadema yalimlenga Zitto, alikuwa atolewe kafara. Yule muuza magazeti aliyepigwa risasi Morogoro akafa, siku hiyo ilikuwa afe Zitto,” alidai Mwampamba.
Alipoulizwa ni kwanini viongozi wa Chadema wanataka kumuua Zitto, alisema ni kwa sababu ya uhusiano mbaya baina yake na vigogo hao ambao chanzo chake ni hatua ya kutaka kugombea urais na kutomuunga mkono Dk. Slaa katika harakati zake za kuwania urais mwaka 2010.
“Zitto hana uhusiano mzuri na viongozi wa juu wa Chadema. Nia yake ya kutaka kugombea urais hawaipendi, inawaudhi sana na amekuwa akitofautiana nao kwa mambo mengi, anajua kuwa anawindwa ndiyo maana hata oparesheni za M4C hashiriki.
“Mimi nilikuwa Chadema na nilikuwa karibu sana na Zitto, najua nini kilikuwa kinaendelea juu yake na najua baadhi ya mambo ya Chadema. Ninaijua mipango ya mauaji ya Chadema. Zitto aliwahi kuwekewa sumu Bagamoyo wakati wabunge wa chama hicho walipokuwa kwenye mkutano wao huko.
“Alinusurika kufa. Alipona baada ya sumu hiyo kutolewa mwilini mwake. Waliiflashi.” Alidai Mwampamba.
Alidai kuwa Zitto alipata kunusurika katika ajali ya gari wakati akitokea Bagamoyo kuelekea Iringa, baada ya gari alilokuwa akitumia kulegezwa nati zinazofunga tairi. Tukio hilo lilitokea muda mfupi baada ya Zitto na Mbowe kutupiana maneno makali kwenye mkutano
Kauli ya Saanane
Akizungumza na Mtanzania Jumatano jana kupitia simu yake ya kiganjani, Saanane alisema madai yaliyotolewa na Shonza na Mwampamba dhidi yake siyo ya kweli, kwa sababu wanayodai kuwa walimkamata akiwa na sumu, hakuwa nao.
Alisema kwa mujibu wa kumbukumbu zake, siku ya Desemba 5, mwaka jana, alikuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akikutana na wanaharakati na baadaye jioni alikwenda harusini.
Hata hivyo, alipoulizwa iwapo alipata kukutana na Shonza na Mwampamba katika Hotel ya Lunch Time, Saanane alisema amepata kukutana nao mara kadhaa kwa ajili ya kupanga mikakati ya PM7, ambayo alishiriki kuianzisha lakini aliachana nao baada ya kubaini walikuwa wakiitumia kwa malengo mabaya.
Mtanzania Jumatano lilipombana Saanane aeleze mikakati waliyokuwa wakiipanga yeye na wenzake katika PM7, alisema ilikuwa ya siri na vikao vyao vilikuwa vya siri kutokana na hofu ya kufikiriwa vibaya na viongozi wa chama iwapo wangebainika wanajihusisha na kundi hilo.
Alipoulizwa kama anafahamiana na Zitto na wapi amekwishakutana naye, alisema anamfahamu na amekuwa akikutana mara kwa mara huku akishangaa tamko lake kwenye mitandao ya kijamii lilikokuwa likieleza kuwa, hamfahamu na hata akimuona anaweza kupishana naye.
Hata hivyo, baadaye Saanane aliomba anuani ya barua pepe ya Mhariri wa gazeti hili na kumtumia barua ya kumtaka amuombe radhi kwa kuandika habari ya uongo iliyokuwa ikieleza madai ya masharika wake wanaomuhusisha na tuhuma za kutumwa kumuwekea sumu Zitto, pasipo kumtafuta Zitto mwenyewe kuzungumza hata neno moja
Vituko vya Dk. Slaa
Dk. Slaa alipotafutwa kwa simu yake ya kiganjani na kuulizwa kuhusu madai hayo, alianza kuporomosha matusi mazito huku akilituhumu gazeti hili kutoa nafasi ya kuandika habari zinazowagusa viongozi wa Chadema badala ya kuandika habari za maendeleo.
“Sina muda wa kujibu maswali hayo… hayana msingi…tuhuma hizo hazijadiliwi kwenye magazeti……ni masuala ya kijinga…pumbavu kabisa. Acheni upumbavu bwana. Nina mambo mengi ya msingi ya kitaifa ya kushughulikia kuliko haya madai ya kipumbavu.” Aling’aka Dk. Slaa.
Hata gazeti hili lilipomsihi awe mtulivu ili aweze kutoa ushirikiano, aliendelea kufoka huku akiporomosha matusi zaidi kabla halijaagana naye na kukata simu.
Alipotafutwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe simu yake iliita muda wote bila majibu na hata Zitto.
EmoticonEmoticon