Desmond Tutu alazwa hospitali

 

Desmond Tutu akiwa kwenye mkutano huko New York nchini Marekani

Kiongozi mashuhuri wa kutetea amani nchini Afrika kusini Desmond Tutu amelazwa hospitali kwa matibabu yanayohusiana na maambukizo sugu mwilini mwake.

Taarifa ya Jumatano kutoka taasisi yake inasema Tutu mwenye umri wa miaka 81 atafanyiwa uchunguzi wa afya ili kutafuta kinachosababisha ugonjwa wake. Taarifa inasema matibabu hayo yasio ya upasuaji yanatarajiwa kuchukua siku tano.

Tutu ambaye  alitumia muda wake wa asubuhi kukaa ofisini kwake kabla ya kupelekwa hospitali ilisemekana alikuwa na hali nzuri.

Mshindi huyo wa tuzo ya Nobel awali alifanyiwa upasuaji wa matibabu ya saratani ya kibofu mwaka 1997 na mara nyingine mwaka 1999.

Tutu anafahamika kama kiongozi wa kitaifa nchini Afrika kusini kwa kupinga kwake utawala wa wazungu walio wachache  nchini humo katika miaka ya 1980. Alishinda tuzo ya amani ya Nobel mwaka 1984 kwa kuikosoa serikali ya kibaguzi na ukiukwaji wa haki uliofanywa chini ya mfumo uliolenga ubaguzi.
Previous
Next Post »