DC akamata wazazi 10 kwa kuficha ‘mafataki’


MKUU wa Wilaya ya Mufindi, Evarista Kalalu amelazimika kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wazazi wa wanafunzi kumi, wanaotuhumiwa kuficha majina ya wanaume ambao wamewapa ujauzito watoto wao ili kupunguza idadi ya wanafunzi wanaokatisha masomo kutokana na mimba.

Wazazi hao waliokamatwa, wanadaiwa kupewa fedha ili kutotaja majina ya wanaume waliowapa mimba watoto wao, kwa kujihusisha na vitendo vya ngono na wanafunzi wa kike ambao wapo katika umri mdogo.

Akizungumza na MTANZANIA, DC Kalalu alisema Serikali ya wilaya hiyo, haitaweza kuendelea kuwavumilia wazazi ambao, wanawafumbia macho wanaume wenye tabia za kujihusisha kimapenzi na wanafunzi.

Bila kuwataja majina yao, alisema tabia za kuchukua fedha kwa watu ambao wanadaiwa kuwapa watoto wao mamba, zinapaswa kukomeshwa kwani kwa kufanya hivyo, tatizo la mimba haliwezi kupungua.

Alisema dawa pekee ya kukomesha vitendo hivyo kwa Wilaya ya Mufindi, ni kuhakikisha wazazi wanasaidia kuwakamata wanaume hao, japo wengi wao wamekuwa wakinyamazishwa kimya kwa kupewa fedha ili kesi zimalizwe.

“Hatuwezi kuvumilia watoto wengi wanakatisha masomo yao kwa mimba huku wanaowapa mimba hizi, wakitoa rushwa kwa wazazi ili kumaliza kesi kimya kimya!.., huu ni mwanzo na tutaendelea hivi ili wengine waogope,” alisema Mkuu huyo wa wilaya.

Aliliagiza Jeshi la Polisi wilayani humo, kuhakikisha wanapita katika shule za sekondari kupata majina ya wanafunzi wa kike ambao wameacha shule kwa sababu za kupata mimba, huku wazazi wao wakimaliza kesi kinyemela licha ya kuwa waliofanya hivyo wanajulikana.

Amewataka wazazi kutoa ushirikiano ili kuwakamata wanaume wanaojihusisha na vitendo vya ngono na wanafunzi wa kike ili kumaliza vitendo hivyo.


Tumaini Msowoya, Mufindi
Previous
Next Post »