Asha Ngulumi:Mpiga debe wa Nyerere, alia kutothaminiwa


Kwa namna inavyoonekana ni kama viongozi nchini wamemsahau, kwani anasema maisha yake yamekuwa magumu. Japo wakati anapigania uhuru hakuwa na tegemeo la kulipwa, lakini anafikiri ni hekima kwa taifa kuwakumbuka watu ambao kwa namna moja ama nyingine walipigania maendeleo ya aina mbalimbali hapa nchini

Naingia katika mtaa wa Hananasif, Kinondoni, nyumba namba 487.

Nakutana na Asha Ngulumbi akiwa ameketi katika chumba chake. Ndiyo kwanza anamaliza dozi ya pili ya dawa za Kifua Kikuu, baada ya ugonjwa huo kumrudia kwa mara ya pili.

Akiwa na umri wa miaka 82 sasa, Asha anayakumbuka yote.

Anasimulia mapenzi yake makubwa kwa chama cha siasa cha TANU, ambacho wakati huo kilikuwa katika harakati za kudai uhuru.

“Nilikuwa na mapenzi makubwa kwa TANU, nilitaka kichukue madaraka na Tanganyika nayo iwe huru,” anasema

Anasema, aliposikia tu kuwa kila Mtanganyika anatakiwa ashiriki katika harakati za kudai uhuru, alihamasika kwa kiasi kikubwa.
“Nilitaka kushiriki kwa namna moja au nyingine katika shughuli za chama,” anasema
 Alichokifanya Asha, ni kwenda katika ofisi za TANU, Kariakoo ambapo alionana na katibu wa tawi aliyefahamika kwa jina la Pili.

“Nilipofika, niliambiwa Chama hakina fedha… na Nyerere anahitajika kwenda Umoja wa Mataifa (UN) kushiriki mkutano wa kudai uhuru,” anasema

Anasema aliangalia hali yake ya kifedha na kujiona hawezi kutoa kiasi kikubwa cha fedha ili kumchangia Nyerere, akaona ni vyema akachangisha.

“Nikaanza kutembea mitaani na kwenye baa kuwahamasisha watu wachange fedha ili tumsaidie Nyerere.Nilipata shida…” anasema

Anasema wakati mwingine alikuwa anatukanwa, anafukuzwa hasa na waarabu wamiliki wa maduka Kariakoo.

“Wahindi walikuwa wananiita ‘goro’ yaani dudu, nikienda kuomba fedha kwa ajili ya Nyerere,” anasema Asha
Previous
Next Post »