POLISI katika Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imetoa masharti ya kuruhusu maandamano ya amani ya kupinga kauli ya kashfa iliyotolewa na raia mmoja wa Uingereza, dhidi ya viongozi wakuu wa nchi.
Maandamano hayo yaliyoandaliwa na Asasi isiyokuwa ya Kiserikali ya Human Settlements of Tanzania (Huseta), yamepangwa kufanyika Jumatano na yataanzia Viwanja vya Mnazi Mmoja na kuishia nje ya Ubalozi wa Uingereza hapa nchini.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi katika Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema hajapata barua ya kuomba kufanyika kwa maandamano hayo. “Lakini nitaangalia maudhui, kama yanafanana na maandamano husika,” alisema.
Alisema akifika ofisini leo na kuiona barua ya kuomba kufanyika, maandamano hayo atakuwa katika nafasi nzuri ya kuzungumzia maandamano hayo.
“Nikipata barua ya maandamano hayo na kuona maudhui yake, nitakuwa katika nafasi ya ama kuyaruhusu au kutoyaruhusu,"alisema Kova
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Huseta, Dagan Kimbwereza, alisema Muingereza huyo (jina linahifadhiwa) amekuwa akitumia mitandao ya kijamii, kuwashfu Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mzengo Pinda.
Mwenyekiti huyo alibainisha kuwa raia huyo wa Uingereza bila ya kuwa na vithibitisho wa kile anachokisema, amekuwa akikashfu mihimili mingine ikiwamo mahakama,tasnia ya habari na wananchi kwa jumla.
“Baada ya kufika ubalozini wawakilishi wawili watawasilisha azimio lenye saini za Watanzania wakiitaka Serikali ya Uingereza kutoa tamko hadharani kwamba yenyewe haihusiki wala haisaidii dharau na maovu mengine yanayofanywa na raia wake dhidi ya Taifa la Tanzania,”alisema Kimbwereza.
Kimbwereza akionyesha kwa waandishi moja ya chapisho ambalo mtuhumiwa ameandika katika mitandao ya jamii ni ile inayosema;
Kikwete aitaka PCCB (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) kupambana na rushwa hadi katika Baraza la mawaziri,’kundi moja la majambazi linaliambia kundi jingine la majambazi kukamata mwizi” .
“Mahakama za Tanzania zimejaa rushwa na hazina uwezo. Rais ndiye msimamizi wa katiba na yeye ndiye mhusika mkuu wa ukiukwaji wa sheria” inasomeka moja ya hoja alizoziandika Sarah katika mitandao ya kijamii.
EmoticonEmoticon