Ukosefu wa maji wawatesa wananchi Mbozi



WANANCHI wa Kijiji cha Shaji Wilaya ya Mbozi Mbeya, wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa maji kutokana na kupungua kwa maji katika Mto Mlowo na Myovizi.
Wakizungumza katika uzinduzi wa jumuia za watumia maji wa bonde la mto Myovizi na Mlowo katika bonde la ziwa Rukwa, walisema kuwa katika mito hiyo maji yamepungua na kwamba ndiyo wanayategemea kwa ajili ya matumizi ya nyumbani,shughuli za kilimo cha umwagiliaji.
“Hali ya mito yetu ni mbaya kwani hakuna maji na hivyo tunakwamishwa katika kufanya shughuli zetu za kila siku,kwani hata majisafi na salama kwa ajili ya matumizi ya kunywa hakuna katika kijiji chetu tunategemea maji ya kisima ambayo hata hivyo tunayafuata umbali mrefu” alisema John Mwansanga.
Akizungumzia hali hiyo,Mkuu wa Wilaya ya Mbozi,Dk Michael Kadeghe alisema wakati mahitaji ya maji yakiongezeka,lakini kiwango cha maji kinazidi kupungua kwa kasi.
Alisema kiasi cha maji kinaendelea kupungua na kuharibiwa na matokeo yake ni kuibuka kwa migogoro ya maji miongoni mwa jamii “Kama hatutakuwa makini katika kuokoa mito hii kutazuka mgogoro mkubwa maji miongoni mwetu.
Dk Kadeghe alisema kumekuwepo na watu ambao wamekuwa wakifanya uharibifu wa maji kwa kuyachafua wakati yanahitajika katika matumizi mbali mbali,huku wengine wakivamia vyanzo vya maji bila kujali athari zinazoweza kutokea hapo baadaye.
Kaimu Ofisa wa Maji bonde la Ziwa Rukwa,Florence Mahay alisema kupungua kwa maji kumesababisha baadhi ya maeneo kutofikiwa kabisa na maji hasa katka ukanda wa chini katika Mto Mlowo.
Alisema uchafuzi wa vyanzo vya maji unatokana na kukithiri kwa shughuli za kibinadamu kama vile ufyatuaji wa matofali na uchomaji moto kandokando ya mito na ulishaji wa mifugo karibu na vyanzo vya maji.
Aidha alisema ili kuweza kukabiliana na changamoto hizo,jumuia hizo za watumia maji zitasaidia kusimamia na uendelezaji wa rasilimaji na kutunza mito na vyanzo vya maji kwa kutumia kanuni na sheria ya usimamizi wa rasilimali za maji namba 11 ya mwaka 2009.     
Previous
Next Post »