'Nilitoa msamaha kwa maslahi ya umma'



WAZIRI wa zamani wa Fedha na Mipango, Basil Mramba, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kuwa aliisamehe kodi kampuni ya M/S Alex Stewart ya nchini Uingereza kwa sababu ya maslahi ya Umma.
Aliyaeleza hayo jana wakati akihojiwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Oswald Tibabyekoma mbele ya jopo la Mahakimu watatu ambao ni Jaji John Utamwa, Jaji Sam Rumanyika na Saul Kinemela.
Mramba kwa pamoja na Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha,Grey Mgonja wanashtakiwa kwa kutumia madaraka yao vibaya kwa kuisamehe kodi Kampuni ya M/S Alex Stewart ya nchini Uingereza ilipokuja kufanya ukaguzi wa madini ya dhahabu na kuisababishia Serikali hasara ya Sh11.7 bilioni.
Akiendelea kujibu hoja za upande wa mashtaka, Mramba alidai kuwa aliisamehe kodi kampuni hiyo kwa kuzingatia maslahi ya umma kwa kuwa kampuni za dhahabu zamani zilikuwa zinauza dhahabu nje na fedha zinabaki huko.
Alidai kuwa baada ya kumpata mkaguzi huyu taifa lilipata faida kwa kujua kiasi cha dhahabu kinachozalishwa, kinachouzwa pamoja na pato la kinachouzwa.
“Kwa mara ya kwanza kungekuwa na utaratibu endelevu wa kukagua migodi ya dhahabu kwa sababu wakati huo kulikuwa hakuna wakaguzi na Watanzania wangefaidika kwa kufundishwa kutokana na kuwapo kwa mkataba huu,”alidai Mramba.
Mramba aliyaeleza hayo, baada ya Wakili Tibabyekoma kumtaka alieleze Mahakama kuwa ni maslahi gani ya Taifa aliyoyazingatia wakati akiisamehe kodi kampuni ya Kampuni ya M/S Alex Stewart?
Baada ya Mramba kujibu swali hilo, Wakili Tibabyekoma alimuuliza kuwa kuhusiana na kodi ambayo kampuni ya M/S Alex Stewart ingeilipa, yeye ameisamehe Serikali ingepata kiasi gani?
Akijibu Mramba alidai kuwa “mtu huyu amekwisha pata msamaha tutamzungumziaje.
Awali akitoa utetezi wake, Mramba alidai kuwa suala la kupata mkaguzi wa dhahabu hapa nchini lilikuwa ni geni ingawa sheria haikuwapo na kwamba halikuhitaji kufanywa kwa pupa, ila agizo la Rais lilikuwa la haraka.
Baada ya Mramba kutoa maelezo hayo, Wakili wa Serikali Mkuu, Fedrick Manyanda alimwonyesha dokezo lilikokuwa likitoka kwake kwenda kwa Waziri wa zamani wa Nisharti na Madini, Daniel Yona na kumuuliza kama analikumbuka?
Akijibu hoja hiyo, Mramba alidai kuwa analikumbuka alikuwa akimshauri waziri mwenzake kwa sababu hakuna waziri anayeweza kumwagiza waziri mwenzake kwa sababu wote wana hadhi sawa, hivyo alikuwa akimshauri.
 
Previous
Next Post »