MWANAMKE ambaye amewaangusha wapinzani wake saba wa kiume kwenye kura za mchujo amelaaniwa na wazee wa kabila lake.
Kundi la wazee wa jamii ya Maasai lilidai kuwa mwanamke kuwa katika uongozi ni laana na kinyume na desturi za Wamasai.
Mwenyekiti wa bodi ya Kampuni ya Huduma za Maji ya Tanathi, Peris Tobiko alishinda tiketi ya TNA kuwania ubunge katika eneo jipya la Kajiado Mashariki.
Wazee hao walihama Chama cha TNA na kuwataka wenyeji wampigie kura mgombea wa ODM ili kuzuia laana kuikumba jamii hiyo.
viongozi wa kidini wa Kaunti ya Kajiado waliwakashifu wazee hao wakisema kitendo hicho kimepitwa na wakati.
Viongozi hao 15 wa makanisa mbalimbali walikutana katika Uwanja wa Sultan Hamud na kufanya maombi ambapo walikemea kitendo hicho wakisema kinalenga kuwatia hofu wagombea wanawake.
Wakiongozwa na Kasisi William Kuturai, viongozi hao walisema hatua hiyo haina nia njema na akawashauri wazee hao wakubali mageuzi miongoni mwa jamii ya Wamaasai na kuwapigia kura viongozi wanaoaminika katika uchaguzi mkuu ujao bila kujali jinsia yao. Tobiko aliwashinda wanaume hao katika uteuzi wa vyama kwa kupata kura 5,328 dhidi ya mpinzani wake wa karibu, Julius Ntayia ambaye alipata kura 2,464.
“Ni makosa kuwatisha watoto wetu. Mungu alitupatia watoto wa kike na kiume; kwa nini tuzime juhudi za mtoto wa kike kwa sababu ya mila na desturi zilizopitwa na wakati?” aliuliza Kasisi Kuturai.
Viongozi hao walisema kumlaani mgombea kunatokana na ushawishi wa ibilisi na kutarudisha nyuma juhudi za Serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na mengine ya kibinadamu kuwaokoa watoto wa kike wa jamii ya Maasai, ambao kwa miaka mingi wamedhulumiwa na mila duni.
“Jambo hili la wazee kuwatisha watu kwa laana halikubaliki katika enzi hizi. Wanafikiri watoto wa kike watafikiria nini?” akauliza aliyekuwa mwenyekiti wa wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Moi, Justus Malit Pileu.
Malit alisema hatua ya wazee hao inalenga kuonyesha kuwa jamii hiyo haina haja na wanawake. “Ni lazima tukubali ukweli na kutoa funzo kwa wazee hawa kwa kumuunga mkono mgombeaji huyo ili kuvunja imani hiyo ambayo imewafunga wanawake Wamaasai tangu zamani,” alisema.
Tobiko alisema hatatishwa na matamshi yaliyotolewa na wazee hao. “Namuomba Mungu awasamehe,” alisema Tobiko.

 
Previous
Next Post »