Mgombea urais nchini Kenya Musalia Mudavadi
MGOMBEA urais nchini Kenya Musalia Mudavadi amesema kuwa endapo atafanikiwa kushinda urais atahakikisha kuwa kesi inayowakabili wachochezi wa machafuko nchini Kenya wakati wa uchaguzi mwaka 2008 itarejeshwa nchini humo.
Alisema kuwa Wakenya hawawezi kuwa wanahangaika kwenda nchi za nje wakati mahakama zao zina uwezo wa kushughulikia kesi hizo.
“ Nilishawahi kulifikisha suala hilo bungeni na mimi nilikuwa mmojawapo kati ya wapiga kura kwa ajili ya kupendekeza kujaribu mahakama iwe ndani ya nchi mwaka 2007” , alisema Mudavadi.
Mudavadi aliyasema hayo mjini Elgeyo Marakwet alipokuwa akihutubia katika mfululizo wa mikutano ya kampeni katika Kata ya Chesoi na Kapsowar alipokuwa akijaribu kuwaunganisha wakenya wote nchini humo.
Wakati huohuo wanasiasa wa Muungano wa Jubilee wameanza kutumia helikopta kwa ajili ya kuwafikia wananchi wao popote pale walipo kwa lengo kwa kujinadi nchini Kenya.
Wiki iliyopita wanasiasa hao waliingia mjini Malindi na viunga vyake,ambapo wananchi wa maeneo hayo walikuwa wakishangilia. Anga za maeneo hayo zilibadilishwa rangi kutoka samawati hadi URP-TNA pale helikopta tatu zilizowabeba vigogo wa muungano huo zilipofuatana kutoka mji hadi kijiji walipokwenda kuhutubia mikutano ya hadhara.
Wengi wa wakazi wa eneo hilo walivutiwa sio sana na vigogo hao bali jinsi walivyotua na kupaa kutoka hapa na pale wakiwaacha wenyeji wakiduwaa jinsi zilivyokuwa zikitumiwa “kama matatu tu.”
Ijapokuwa mji wa Malindi una uwanja wa ndege, si kawaida ndege za helikopta kutua nyingi kwa pamoja jinsi ilivyokuwa hapo Jumamosi.
Helikopta tatu zilizopakwa rangi maridadi zilitua uwanjani hapo moja baada ya nyingine, ya kwanza ni ile iliyochorwa na kurembeshwa kwa rangi za chama cha United Republican Party (URP) iliyombeba mgombea makamu wa rais wa muungano wa Jubilee William Ruto.
Punde tu baada ya helikopta hiyo kutua, ilifuatwa kwa karibu na ile ya rangi nyekundu na nyeupe za TNA ambayo ilimbeba mgombea wa urais Uhuru Kenyatta. Mda mfupi baadaye , ndege ya tatu ilitua yenye rangi ya samawati.
Watu walishangaa inambeba nani lakini walishikwa na kiwewe pale mgombea useneta wa jiji la Nairobi Mike Mbuvi Sonko alipoonekana akishuka kutoka ndege hiyo. Kisha ndege hizo baadaye zilifuatana kwenda uwanja wa Barani kulikokuwa na mkutano huo. Uwanja wa ndege wa Malindi na Barani ni kama kilomita moja tu.
Lakini ndege hizo kwanza zilizunguka angani kwenye mji huo wa kitalii kama vile kufanya kinachoitwa na wazungu “lap of honour” kabla kutua uwanjani hapo huku umati ukishangilia kwa nderemo na nduru.a
EmoticonEmoticon