Ndege ya Syria ilikuwa na mizigo haramu


 

Maafisa wa Uturuki wamesema kuwa ndege ya abiria ya Syria ambayo ilikuwa inapita katika anga yake kutoka Moscow kuelekea Damascus, kinyume na sheria, ilikuwa imebeba mizigo haramu

Ndege za kivita za Uturuki zililazimisha ndege hiyo ya abiria kutoka Syria kutua katika uwanja wa ndege wa Ankara

Ndege hiyo iliruhusiwa baadaye kuendelea na safari lakini maafisa wa Uturuki walisema wamenasa baadhi ya mizigo iliyokuwa imebebwa na ndege hiyo ili kuifanyia uchunguzi.

Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Uturuki, Ahmet Davutoglu, amethibitisha kunaswa kwa baadhi ya mizigo iliyokuwa ndani ya ndege hiyo na vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa mizigo hiyo huenda ilikuwa ni vifaa vya mawasiliano.

Awali bwana Davutoglu alisema kuwa uturuki ilikuwa imejitolea kukomesha usafirishaji silaha wa aina yoyote nchini Syria kupitia anga yake.

Tukio hilo linajiri wakati Syria na Uturuki zikiendelea kufyatuliana mizinga katika maeneo ya mpakani.

Urusi imetaka Uturuki kutoa maelezo kuhusu hatua yake na kuituhumu Ankara kwa kuhatarisha maisha ya raia wake.
Hata hivyo waziri Davutoglu amesema kuwa Uturuki itaendelea kuchunguza ndege za Urusi ambazo zinapita katika anga yake.

Hali ya taharuki imetanda kati ya nchi hizo mbili tangu raia watato wa Uturuki kuuawa wiki jana katika shambulizi la makombora katika eneo la mpaka wa nchi hizo mbili.

Kwa jibu lake, Uturuki nayo ilishambulia Syria kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa mgogoro wa kisiasa nchini humo mwaka jana kumtaka rais Bashar Al Assad kuondoka mamlakani.

Uturuki iliiwekea vikwazo vya silaha Syria mwezi Septemba

Previous
Next Post »