Mgombea wa kiti cha urais kwa
tiketi ya chama cha Republican , Mitt Romney, amemtaka mwanasiasa
mwenzake wa chama hicho kujiondoa katika kinyang'anyiro cha uchaguzi wa
kiti cha Useneta baada ya kutoa matamshi yaliyozua utata kuhusu ubakaji.
Todd Akin, ambaye ni mwanasiasa wa bunge la
Congress alizua manung'uniko kwa kudai kuwa mwili wa mwanamke una uwezo
wa kuzuia mimba katika baadhi ya matukio ya ubakaji.
Matamshi
ya Todd Kin anayegombea kiti cha seneta nchini Marekani yalitolewa
wakati wa mahojiano. Alikuwa akitetea msimamo wake dhidi ya utoaji
mimba.
Alipoulizwa kuhusu kutoa mimba iwapo mwanamke
atabakwa, Todd Kin alieleza kuwa katika ubakaji halali au kile
alichokitaja kuwa 'legitimate rape' kuna uwezekano kwamba kibiolioia,
mwili wa mwanamke utamzuia kupata mimba anapobakwa.
Matamshi yake yamezua hisia kali. Mpinzani
wake Mitt Romney amesema, ''Matamshi yake kuhusu ubakaji yanaudhi sana
na siwezi nikatetea msimao wake au nikamtetea yeye''
Baadhi ya wenzake Todd Akin kutoka chama cha Republican wamemtaka kujiondoa kwenye kinyang'anyiro cha kuwania kiti cha useneta.
Hiki ni kipindi kigumu kwa wana Republican ambao
walikuwa wamejiandaa kuendeleza kampeni yao kwa kumshambulia rais Obama
kwa jinsi uchumi ulivyozorota wakati wa uongozi wake. Badala yake sasa
wamejikuta wakirushiana maneno kuhusu sera za kijamii.
Chama cha Democrats kimechukua fursa hiyo
kushambulia Republicans kwa kuwataja kama watu ambao hawazingatii
maslahi na hisia za wanawake.
Todd Akin ameomba msamaha kufuatia matamshi yake.
"Nilitumia maneno yasiofaa na ninaomba msamaha.
Nina watoto wawili wa kike na nataka haki kutendeka, nina roho ya huruma
kwa waathiriwa wa ubakaji na nawaombea. Ukweli ni kuwa, mtu anaweza
akapata mimba kutokana na ubakaji. Ukweli ni kwamba, kuna waathiriwa
wengi wa ubakaji. Makosa yangu ni kutumia maneno yasiofaa. Naomba
msamaha wako. ''
Hata hivyo halitakuwa jambo la kushangaza iwapo
atalazimika kujiondoa kwenye mbio za kuwania kiti cha useneta kwa sababu
ya matamshi hayo.
EmoticonEmoticon