WATU WANNE WANAOSADIKIWA KUWA NI MAJAMBAZI WAMEUAWA NA POLISI KATIKA ENEO LA CHEKERENI MPAKANI MWA WILAYA YA ARUMERU JIJINI ARUSHA













WATU wanne wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wameuwawa kwa katika mapambano ya majibizano ya risasi katika eneo la Chekereni mpakani mwa Wilaya ya Arumeru na Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani humo, Liberatus Sabas, Jeshi hilo lilipokea taarifa za kiintelejensia Septemba 17, 2015 juu ya kuwepo kwa kundi la majambazi lililotaka kufanya uvamizi na uporaji ndani ya jiji la Arusha.
Katika tukio hilo, amesema walipata taarifa za uwepo wa kundi la majambazi toka nchini Kenya tangu mwezi Agosti 19, 2015 kuwa wangeshirikiana na wahalifu wengine wa hapa nchini kufanya uhalifu kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo taasisi za fedha.
“Baada ya taarifa tuliendelea na ufuatiliaji na kufanikiwa kumkamata mtu aitwaye Sixtus Ngowi (51), Mtanzania, mkazi wa Ngulelo jijini hapa na baada ya mahojiano alikiri kushirikiana na majambazi wenzake wa nchini Kenya katika kufanya matukio mbalimbali ya kiuhalifu nchini”

Mtuhumiwa huyo alikiri kushiriki baadhi ya matukio ikiwa ni pamoja na tukio la uporaji wa fedha zaidi ya dola 2,000,000 tukio lililotokea Jijini Dar es salaam mwaka 2005 kwenye Kampuni ya Security Group 4 na kisha kufikishwa Mahakamani.
Aidha, mwaka 2002 alihusika na tukio la uvamizi wa Benki ya NBC tawi la Moshi mkoani Kilimanjaro. Mwaka 2014 jambazi huyo aliwahi kushtakiwa nchini Kenya kwa matukio ya uhalifu katika Mahakama ya Mlimani Law Court iliyopo Nairobi nchini Kenya lakini baadae aliachiwa huru.
Mbali na matukio hayo, jambazi huyo alikiri kuhusika katika matukio kadhaa ya ujambazi akishirikiana na wenzake ikiwemo matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha katika mkoani Arusha kwa wafanyabiashara wakubwa wa madini ya Tanzanite na hoteli za kitalii.
Miongoni mwa tukio walilolifanya ni kumjeruhi mfanyabiashara wa madini, Mathius Manga, ambaye alipigwa risasi kwenye ubavu wa kulia.
Siku ya jana jambazi huyo aliwatonya Polisi juu ya tukio walilokuwa wanataka kulifanya katika kufanikisha juu ya upatikanaji wa wenzake ambao siku ya jana walipanga kuvamia katika duka la kubadilishia fedha liitwalo Sanya lililopo jijini Arusha.
Walipokuwa wanaelekea eneo la tukio akiongozana na Askari Polisi kwa nia ya kufanikisha kuwapata majamabzi wengine, baada ya kufika eneo la tukio (kabla hawajawakamata) majambazi hao ambao walikuwa kwenye gari aina ya Noah yenye namba za T. 981 AVK walishtuka na kuanza kulishambulia gari lililokuwa na askari Polisi na kumjeruhi mwenzao Sixtus Alfedy Ngowi ambaye alifariki muda mfupi wakati akiwa njiani kupelekwa hospitali.
Kamanda Sabas, amesema Polisi walijibu mapigo na kufanikiwa kuwaua majambazi watatu huku wengine wakifanikiwa kukimbia na katika upekuzi kila mmoja alikutwa na bastola pamoja na risasi. Pia walikuta mabegi matatu meusi ambapo ndani yake kulikuwa na bunduki mbili aina ya AK 47 zenye namba 83 LG 3953 56-1 na nyingine yenye maandishi ya kirusi pamoja na SMG moja yenye namba 56-1 28038394.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Liberatus Sabas, akiwaonyesha waandishi wa habari silaha zilizokutwa toka kwa majambazi hao pamoja Bullet Proof.
Bastola ambazo zilikutwa toka kwa majambazi hao zilikuwa na namba CZ 75 Compact Luger-9mm, namba A. 269206, CZ 85 B Luger 9mm, namba 051967 na Chines Pistol namba 967741. Pia zilipatikana magazine nne tupu za SMG, risasi 85 za SMG/AK 47 na risasi 28 za bastola.
Mbali na silaha hizo pia walikutwa na 'Radio Call' mbili aina ya Kenwood zilizokuwa hewani na wimbi la Polisi Arusha, bullet proof moja, vifaa vya kusafishia bunduki, mifuko mitatu ya kubebea pesa na vifaa vingine.
Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru ambapo walikutwa pia na vitambulisho mbalimbali vya Jamhuri ya watu wa Kenya pamoja na simu tano aina ya Nokia, Tecno na Samsung.
Jeshi la Polisi linaendelea na upelelezi juu ya tukio hilo ikiwa ni pamoja na kuwatafuta watuhumiwa wengine waliofanikiwa kukimbia na kubaini mtandao mzima wa kundi hilo.
Previous
Next Post »