Kina mama
na watoto wakiwa wamelala wakisubiri kujiandikisha kwenye daftari la
kudumu la wapigakura katika Kituo cha Ulongoni, Gongo la Mboto, Dar es
Salaam jana. Picha na Venance Nestory
Wakati
uandikishaji wa wananchi katika Daftari la Kudumu la Wapigakura,
ukiingia siku ya tatu leo, kasoro lukuki zimeendelea kugubika mchakato
huo huku katika baadhi ya vituo wananchi wakizichapa wakigombania
kuingia chumba cha kujiandikisha.
Tukio la
kutwangana makonde lilitokea katika Kituo cha Shule ya Mwangaza, Gongo
la Mboto saa 2.15 asubuhi wakati uandikishaji ulipokuwa ukianza.
Mashuhuda
wa tukio hilo walisema: “Polisi unaowaona wamefika muda si mrefu, wala
hawakuwepo hapa tangu asubuhi... ninadhani walipewa taarifa baada ya
watu kuanza fujo wakigombania kuingia ndani kujiandikisha,” alisema
Magreth John na kuongeza:
“Watu
wamepigana kwa sababu wanasema kuna wenzao ambao majina yao
hayakuandikwa jana (juzi) halafu wamefika asubuhi wakaanza kuitwa ndani
kujiandikisha. Hapo ndipo mzozo ulipoanzisha na ngumi zikafumuka.”
Msimamizi wa kituo hicho, Ramadhani Mshindo alisema mzozo huo ulitokea kwa sababu ya wananchi hao hawakuelewa utaratibu.
“Jana
(juzi) jioni wakati tunafunga zoezi hili saa 12.00 jioni kuna watu wengi
walikuwa kwenye foleni ambao hawakuandikishwa, kwa hiyo tuliwaandika
majina ili leo (jana) wakifika hapa watangulie kuandikishwa kabla ya
wengine. Sasa tulivyofika na kuanza kuita majina yao ili waingie
kujiandikisha ndipo watu wakaanza fujo na kupigana ikabidi tupige simu
polisi ili waje kutuliza ghasia,” alisema Mshindo.
Katika
Kituo cha Shule ya Msingi Jica, Tabata wananchi walilalamikia suala la
muda kwani waandikishaji walichelewa na hadi saa 4.30 asubuhi, asilimia
kubwa ya watu hawakuwa wamepata huduma. “Nimefika hapa saa 12.00 asubuhi
lakini hadi sasa sioni dalili ya kuandikishwa leo... Wametuambia
wanaanza kuandikisha wale waliobaki jana kwa sababu majina yao
yaliandikwa kwa hiyo sisi wa leo tunasubiri kwanza,” alisema Maria
Saleh.
Maria alisema uandikishaji unakwenda taratibu kutoka na mashine kugoma mara kwa mara.
Malalamiko
kama hayo yalitolewa na wananchi waliokuwa wamefika kujiandikisha
katika Kituo cha Shule ya Msingi, Ulongoni, Gongo la Mboto na waandishi
wetu walishuhudia watu wengi wakiwa kwenye misururu, wengine wakiwa
wamelala pembeni ya kituo hicho baada ya kuchoka kusimama muda mrefu.
Hata
hivyo, kwenye kituo hicho, wananchi walijiwekea utaratibu kwamba kila
mtu anayefika anaandika namba kwenye daftari na kupewa kikaratasi kidogo
chenye namba hiyo ndipo anapanga foleni.
Utaratibu ambao ulisaidia kupunguza usumbufu na kuondoa vuta ni kuvute wakati wa kuingia kwenye chumba cha kujiandikisha.
Lakini licha ya kujiweka utaratibu huo, Ibrahim Kitumbi alisema changamoto ya muda na vifaa ilikuwa palepale.
“Hivi
tunavyozungumza watu waliyopewa namba wamefika 2,145. Hawa wameandika
majina tu na kupewa namba. Waliojiandikisha tangu jana hawafiki hata
200. Sasa kwa siku nane zilizobaki kweli tunaweza kumaliza kuandikishwa!
Huku si kutunyima haki?” alihoji.
Wakati
wananchi wakitoa malalamiko hayo, Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Ulongoni,
Majura Mtalemwa alisema zoezi la uandikishaji linakwenda vizuri tofauti
na wananchi wanavyolilalamikia.
Mkazi wa
Temeke, Steven Almasi aliyefika kujiandikisha katika Kituo cha Magogoni,
Yombo alisema mwaka huu wa uchaguzi kuna uwezekano mkubwa wa baadhi ya
wananchi kutoshiriki uchaguzi.
Mtendaji wa mtaa huo, Zeddy Zeddy alikiri kuwapo baadhi changamoto kwenye kituo chake ikiwamo uchache wa mashine za kuandikisha.
“Mwitiko
wa watu umekuwa mkubwa tofauti na matarajio yetu kwa hiyo kama mashine
zikiongezwa kwenye baadhi ya vituo, itasaidia kuondoa msongamano na kazi
kukamilika kwa wakati,” alisema Zeddy.
“Kama
Tume ingeongeza mashine, mambo yangekwenda vizuri zaidi lakini
kinachoendelea ni ngumu kusema kuwa watu wote wataandikishwa kama
ilivyopangwa,” alisema mtaalamu wa BVR aliyekuwapo Kituo cha Shule ya
Msingi Kibangu, Ubungo, Suleiman Mahmoud.
Katika
kituo cha Kontena – Tanesco, Kinondoni ni mashine moja tu iliyokuwa
ikifanya kazi kati ya tatu kutokana na kuharibika licha ya idadi ya watu
kuwa wachache.
“Mashine
moja ilikuwa haifanyi kazi hadi saa tatu asubuhi, wameleta nyingine
lakini nayo kamera inasumbua. Hii yangu printa haifanyi kazi hivyo ipo
moja tu. Tumewapigia IT (mafundi wa Teknolojia ya Mawasiliano) wamesema
wanakuja lakini wengi wanatembea kwa miguu wanachelewa kufika,” alisema
mwendeshaji mashine ya BVR kituoni hapo, Max Phillipo.
Mkazi wa
Mwananyamala, Hemed Shefaya alisema alifika kituoni tangu saa 10
alfajiri akiwa na wenzake watatu lakini kilifunguliwa saa 2.30 asubuhi.
“Mashine
hizi zinaharibika mara kwa mara, kwa sasa wamezitengeneza lakini mikono
ya wasimamizi ni mizito sana. Tulikuja jana na kupatiwa namba lakini
hatukufanikiwa kuandikishwa... fikiria mimi namba 18 ya jana nimekuja
saa 12 asubuhi lakini bado hadi sasa (saa 5.43) sijaandikishwa,” alisema
Ramadhani Mkombozi aliyekuwa katika Kituo cha Shule ya Msingi Kisiwani,
Mwananyamala.
Ofisa
Uchaguzi wa Manispaa ya Kinondoni, Valence Urassa alisema tatizo la
kuharibika kwa BVR lilikuwa likifanyiwa kazi na mafundi wa NEC na
Manispaa na kwamba maeneo yenye wakazi wengi yalikuwa yakiongezwa
mashine kufikia mbili kila kituo.
Kuhusu
kuchelewesha kufungua vituo, alisema kituo chochote hakitafunguliwa 2.00
asubuhi iwapo waandikishaji hawatakuwa wamekamilisha maandalizi ya
vifaa na kuandikisha kwani kuwahisha kutaleta matatizo.
Baadhi ya wasimamizi wametoa wito kwa NEC kuongeza vifaa pamoja na wataalamu ili kazi hiyo ikamilike kwa wakati.
Msimamizi
wa Kituo cha Chuo cha Usafirishaji (NIT), Kelvin Donald alisema mashine
alizonazo zinasumbua tangu juzi na hata baada ya kutoa taarifa na
kubadilishiwa bado tatizo hilo linaendelea.
“Kwa wastani wanajitokeza watu 1,200 kila siku na hapa tuna mashine tano tu, moja haifanyi kazi,” alisema Donald.
Mwenyekiti
wa Serikali ya Mtaa wa Mbezi Luis, Omari Mshauri alisema baada ya umeme
kuwa kikwazo, juzi msamaria mmoja alijitolea jenereta huku wengine
wakichangia mafuta kuendelea na kazi.
NEC yafafanua
Mkurugenzi
wa Uchaguzi wa NEC, Julius Malaba alisema wakazi wote wa jiji hili
waliojitokeza wataandikishwa hata baada ya siku zilizopangwa kumalizika
hivyo hawatakiwi kuwa na hofu.
“Hakuna
mtu aliyejitokeza kuandikishwa halafu akaachwa... tutaandikisha mpaka
wote waliojitokeza siku ya mwisho watakapokamilika.
“Mpaka
sasa tuna mashine takriban 3,500 na nyingine zinaendelea kuingia kutoka
mikoa ambayo tumeshakamilisha kuandikisha. Hizi zote zitaletwa kuongeza
nguvu ya uandikishaji katika maeneo yenye wakazi wengi na kumaliza
haraka,” alisema Malaba.
Kawe kujiandikisha upya
Malaba
alieleza kuwa wakazi wa Jimbo la Kawe ambao walijiandikisha awali katika
uandikishaji wa majaribio, watatakiwa kujiandikisha upya ili wapate
vitambulisho vya sasa.
Hata hivyo, hakutaja sababu za kurudia na kuahidi kufafanua zaidi leo.
RC atoa maagizo
Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik amewataka wakurugenzi wote wa
Manispaa za Dar es Salaam kutoka maofisini na kwenda kusimamia kwa
karibu uandikishaji huo na kutatua matatizo yanayoripotiwa na wananchi
kila wakati.
Alisema
amepokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi, mojawapo likiwa
waandikishaji kuchelewa kufika vituoni, kuwahi kuondoka kabla ya muda na
mashine kugoma.
“Tutachukua
hatua kali kwa ofisa mwandikishaji yeyote atakayekiuka taratibu na
kukwamisha uandikishaji... tunafahamu uandikishaji unakabiliwa na
changamoto nyingi, lakini nimepata taarifa kuwa waandikishaji pia
wanahujumu uandikishaji bila sababu za msingi,” alisema Sadik.
Chanzo:Mwananchi
EmoticonEmoticon