Rais Kikwete Awashangaa Wanasiasa Wanaokosoa Kitendo cha Serikali Yake Kukopa Fedha Nje


RAIS Jakaya Kikwete amewashangaa wanasiasa wanaokosoa kitendo cha Serikali yake kukopa fedha nje ya nchi kuwa kinazidisha deni la taifa, kwamba hawana ufahamu na kufafanua kuwa katika kuharakisha maendeleo ya nchi, kukopa ni jambo la kawaida.
 
Alisema hata mataifa makubwa yaliyopiga hatua kubwa kwenye maendeleo yamekuwa yanakopa na akasisitiza kuwa uamuzi wa serikali kwenda nje kukopa amekuwa anaufanya ili kupata fedha kwa ajili ya kujenga miundombinu ambayo itaifanya nchi ipige hatua kubwa kimaendeleo.
 
Alitoa mfano kuwa hata kama mtu anaeendesha duka ni lazima akakope benki kama anataka kuendeleza duka lake, kama hatafanya hivyo kwa kuamini kuwa fedha anazopata kwa kuuza bidhaa zitalitunisha duka hilo basi asubiri miujiza ya kumpatia faida.
 
Aliyasema hayo wakati akizungumzia uamuzi wa serikali yake kuwenda kukopa nje kwa ajili ya kujenga miundombinu mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa mkongo wa taifa ambao alisema lengo lake ni kuweka misingi ya miundombinu wakati taifa linapoelekea kwenye utekelezaji wa ujenzi wa viwanda vya kisasa.
 
Rais Kikwete alisema baada ya kufanya uamuzi huo aliamua pia kuwekeza kwenye utafiti kwa kuhakikisha kuwa Serikal inatenga fedha kwa ajili ya kuwasomesha watafiti, kununua vifaa vya utafiti na kukarabati vituo vya utafiti ambayo alisema vingi vilikuwa kwenye hali mbaya.
 
“Tulianza na Sh bilioni 10, tunashukuru sasa hivi tupo kwenye Sh bilioni 60 na naamini kuwa Rais atakayekuja ataendeleze juhudi hizi kwa kutenga fedha zaidi kwa ajili ya tafiti maana nikiangalia hali ya baadaye ya maendeleo ya nchi hii inategemea watafiti, wanasayansi na wabunifu,” alisema Rais Kikwete.
 
Rais alisema anajivuna kwamba anaondoka madarakani wakati shughuli za utafiti zimepata uhai na kwamba juhudi zilizofanywa na Serikali yake za kuwaendeleza wabunifu zimezaa matunda mengi kwani kwa sasa nchi ina watafiti wazee na vijana wanaofanya mambo makubwa yanayotambulika kimataifa.
 
Alisema fedha zilizotolewa na serikali yake zimesaidia kusomesha watafiti 517 katika kozi za shahada ya uzamili na uzamivu na vituo 20 vimekarabatiwa na miradi 70 ya utafiti imetekelezwa.
 
“Ndio maana nasema kiongozi anayekuja asipoliendeleza hili, mwambieni mzee unatuletea matatizo.”
 
Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dk Hassan Mshinda alisema kongamano hilo la nne limewakusanya wanasayansi, watafiti, watunga sera na wabunifu mbalimbali.
 
Alisema mada 80 zitajadiliwa ikiwemo tafiti mbalimbali zilizofanywa na watafiti wa ndani, kujadiliana changamoto za kupeleka utafiti sokoni na upatikanaji wa teknolojia na jinsi ya kuhuisha sayansi asili na sayansi ya kisasa.
 
Dk Mshinda alimshukuru Rais Kikwete kwa kujali na kuwapa umuhimu watafiti kuliko miaka ya nyuma na akasema kuwa anaamini kuwa msingi uliowekwa utaendelezwa na awamu ijayo.
 
Alisema juhudi zilzofanyuwa na Rais Kikwete zimeungwa mkono na nchi za Sweden na Finland ambao nao sasa wameamua kutoa fedha kusaidia juhudi za serikali katika kufanya tafiti.
Previous
Next Post »