Mh.Mkapa ameziasa nchi za Afrika kuacha kutegemea misaada ya wahisani.


Rais mstaafu wa serikali ya awamu ya tatu Mh.Benjamin Mkapa amezitaka nchi za kiafrika kuacha kutegemea zaidi misaada ya wahisani toka ng’ambo kwani baadhi ya nchi hizo zimeanza kuchoka kutokana na kuelewemewa na madeni makubwa, badala yake amezishauri nchi za Afrika kujiwezesha kwa mambo yaliyo ndani ya uwezo wa waafrika wenyewe ikiwemo kufanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa.
Mh. Mkapa ametoa changamoto hiyo wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 19 tangu kuanzishwa kwa radio maria Tanzania, sherehe zilizofanyikia katika kanisa katoliki parokia ya madhabahu ya bikira maria kawekamo jijini Mwanza ambapo rais huyo mstaafu pia ameongoza harambee kwa ajili ya kuchangia kiasi cha shilingi milioni 60 zinazohitajika kuendesha radio hiyo na kufanikisha kupatikana kwa zaidi ya shilingi milioni 40 zilizochangwa kwa njia mbalimbali na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.
 
Rais huyo mstaafu Benjamin Mkapa pia amegusia suala la uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika oktoba 25 mwaka huu kwa kutoa tahadhari kwa baadhi ya wanasiasa wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi.
 
Awali akihubiri katika ibada ya misa takatifu iliyohudhuriwa na mamia ya waumini pamoja na mahujaji 400 waliotoka hija katika eneo la nyakibeho nchini Rwanda askofu mkuu wa kanisa katoliki jimbo kuu la Mwanza mhashamu Thadeus Rwaichi amesema kuwa taifa na kanisa la mungu linapoelekea kwenye uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani zipo changamoto nyingi zinazolikabili na ambazo zinahitaji waumini kusimama katika imani ya kweli na dhabiti.
Previous
Next Post »