
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amefanya uteuzi wa wakuu wapya wanne wa Mikoa, amewahamisha wengine sita
na ameamua kuwa wengine watatu watapangiwa kazi nyingine.
Taarifa
iliyotolewa mjini Dodoma jioni ya leo, Jumatano, Novemba 5, 2014 na
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue inasema kuwa, Wakuu wapya wa
Mikoa ni Bi. Halima Omari Dendego ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara,
Dkt. Ibrahim Hamisi Msengi ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Bi.
Amina Juma Masenza ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa na Bwana John
Vianney Mongella ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera.
Taarifa
inasema kuwa kabla ya uteuzi wake Bi. Dendego alikuwa Mkuu wa Wilaya ya
Tanga, Dkt. Msengi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Bi. Masenza alikuwa
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela na Bwana Mongella alikuwa Mkuu wa Wilaya ya
Arusha.
Taarifa
hiyo inasema kuwa Wakuu hao wapya wa Mikoa wataapishwa kesho, Alhamisi,
Novemba 6, 2014 saa saba mchana, Ikulu, Dar es Salaam.
Aidha,
taarifa hiyo imesema kuwa Wakuu wa Mikoa ambao watapangiwa kazi
nyingine ni Kanali (Mst) Fabian Massawe wa Kagera, Dkt. Christine
Ishengoma wa Iringa na Kanali Joseph Simbakalia wa Mtwara.
Wakuu
wa Mikoa ambao wamehamishwa vituo vya kazi ni Bwana Magesa S. Mulongo
ambaye anakwenda Mkoa wa Mwanza kutoka Arusha, Dkt. Rehema Nchimbi
ambaye anakwenda Mkoa wa Njombe kutoka Dodoma, Bwana Ludovick John
Mwananzila anakwenda Tabora kutoka Lindi, Kepteni (Mst) Anseri Msangi
anayekwenda Mkoa wa Mara kutoka Njombe na Mhandisi Everist Ndikilo
ambaye anakwenda Arusha kutoka Mwanza.
Wengine
waliohamishwa ni Luteni (Mst) Chiku A.S. Galawa ambaye anakuwa Mkuu wa
Mkoa wa Dodoma kutoka Tanga, Dkt. Rajab Rutengwe ambaye anakwenda Mkoa
wa Tanga kutoka Katavi, Bi Fatma Mwasa ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa
Geita kutoka Tabora na Bwana Magalula S. Magalula ambaye anahamishiwa
Lindi kutoka Geita.
Taarifa
hiyo imesema kuwa Wakuu wa Mikoa ya Dar es Salaam, Kigoma, Kilimanjaro,
Manyara, Mbeya,Morogoro, Pwani, Rukwa, Shinyanga, Ruvuma, Singida na
Simiyu watabakia kwenye vituo vyao vya sasa.
Aidha, Rais Kikwete amefanya uteuzi wa Wakuu wapya wa Wilaya, kuhamisha baadhi yao na kutengua uteuzi wa baadhi.
Taarifa kamili itatolewa na Waziri Mkuu baada ya kuwa wamepangiwa vituo vya kazi.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
05 Novemba,2014
EmoticonEmoticon