MWANAFUNZI DARASA LA NNE AKATWA MAPANGA NA MFANYAKAZI WA NYUMBANI



Mama mzazi akiwa na Mwanafunzi wa darasa la nne wa shule ya msingi Motomoto kata ya Vumilia wilayani Urambo aliyekatwakatwa mapanga na mfanyakazi wa nyumbani kwa madai ya kunyimwa hela na baba mzazi wa mtoto hu
========  =======  =======
Na Allan Ntana, Urambo

MTOTO Perezi Christian (12) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya msingi Motomoto iliyoko katika kata ya Vumilia wilaya ya Urambo mkoani Tabora amekatwakatwa  mapanga mikononi na miguuni na   mfanyakazi wa nyumbani.

Akizungumza kwa masikitiko makubwa akiwa wodini alikolazwa Perezi mama mzazi wa mtoto huyo Regina Fumbo (45) ambaye ni muuguzi katika kituo cha afya Zogolo kilichoko katika tarafa ya Nyasa wilayani Nzega alisema mtoto wake amekatwakatwa mapanga na mfanyakazi wa shambani anayeitwa Abdallah Alfan muha mwenye umri wa kati ya miaka 39-44.

Alisema awali hapakuwa na ugomvi wowote kabisa kila alichotaka alikuwa anapewa, alichukua uamuzi huo kwa hasira tu kwani tayari alikuwa ameahidiwa kulipwa hela alizokuwa ameomba kwa bosi wake ambaye ni baba mzazi wa mtoto huyo Bw. Christian Mlela.

‘Hili tukio limenisikitisha sana, nilipigiwa simu nikiwa kazini kwangu kule Nzega, nikajua mtoto wangu sitamkuta hai tena, nilikuja mbio mpaka wodi ya wanaume alipolazawa, kwa kweli hali yake haikuwa nzuri, namshukuru Mungu sasa hivi anaendelea vizuri, na huyo mtuhumiwa ameshakamatwa na polisi’, alisema.


Mtoto Perezi alipohojiwa na mwandishi wa gazeti hili akiwa wodini katika hospitali ya wilaya Urambo alisema kabla ya kukatwa mapanga babake hakuwepo, mtuhumiwa huyo alipokuja alidai baba hataki kumpa hela yake yeye anajali kazi zake tu, sasa ngojea, ndipo akaanza kumkata kata.


‘Ninaumia sana, sijui kama nitapona ili niendelee na shule kama nilivyokuwa, jamani naomba madaktari wanisaidie nipone haraka kabla shule hazijafunguliwa mwezi ujao’, alisema mtoto Perezi  kwa masikitiko makubwa mbele ya mwandishi.


Baba mzazi wa Perezi ambaye ni Katibu Meneja wa Chama cha Msingi Kasela katika kijiji cha Motomoto alipohojiwa na mwandishi wa gazeti hili alidai walikuwa wamekubaliana amlipe sh 200,000 watakapouza tumbaku msimu huu na tayari walikuwa wameshaikausha hivyo wakawa wanasubiri kupima uzito wake na kujua gredi ili wakauze.


‘Huyu bwana alianza kunidai hela hata kabla ya kuuza tumbaku kama tulivyokubaliana, nikamwomba avumilie kidogo ili nimtafutie kwani yeye alidai anataka kurudi kwao Kigoma, lakini awali nilimpa hela kidogo za kujikimu kiasi cha sh 20,000’, aliongeza.


Aidha aliongeza kuwa tayari wameshatoa taarifa kituo cha polisi Urambo na mtuhumiwa huyo anashikiliwa na jeshi la polisi kwa ajili ya hatua zingine za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani.
Previous
Next Post »