TUME YA WARIOBA YAVUNJWA RASMI


kikwete_15d33.jpg

Rais Jakaya Kikwete ameivunja rasmi Tume ya Mabadiliko ya Katiba, baada ya kukamilisha kazi yake, ikiwa ni pamoja na kuwasilisha Rasimu ya Pili ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 2013 katika Bunge Maalumu la Katiba wiki iliyopita.
Tume hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba ilikusanya maoni ya wananchi kwa zaidi ya miezi sita na hatimaye kuandaa rasimu ya kwanza na ya pili, ambayo inatarajiwa kuanza kujadiliwa katika Bunge hilo wakati wowote kuanzia sasa.
Rasimu hiyo itajadiliwa na Bunge hilo baada ya kuwasilishwa na Jaji Warioba, Machi 18, mwaka huu.
Kuvunjwa kwa Tume hiyo kulitangazwa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, jijini Dar es Salaam jana.Kwa mujibu wa taarifa ya kurugenzi hiyo, hatua hiyo ilichukuliwa na Rais Kikwete Machi 19, kwa Tangazo la Serikali namba 81 la Machi 21, mwaka huu, ikiwa ni siku moja tu baada ya Jaji Warioba kuwasilisha rasimu hiyo katika Bunge hilo.
Hatua hiyo ilichukuliwa na Rais Kikwete kwa mujibu wa kifungu cha 31 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2012.
"Hivyo kwa Tangazo hilo, shughuli zote za Tume ya Mabadiliko ya Katiba zimemalizika rasmi tarehe 19 Machi, 2014," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu.
Tume hiyo iliundwa na Rais Kikwete kwa mujibu wa kifungu cha 5 na 6 cha sheria hiyo, sura ya 83 kwa Tangazo la Serikali namba 110 la mwaka 2012.
Tume hiyo iliyokuwa na wajumbe 30; wakiwamo 15 kutoka Tanzania Bara na 15 kutoka Zanzibar, ilitangazwa na Rais Kikwete, Aprili 6 na kuapishwa Aprili 13, mwaka jana.
Iliongozwa na Jaji Warioba akisaidiwa na Makamu wake, Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhan.
Wajumbe wengine kwa upande wa Tanzania Bara, ni Profesa Mwesiga Baregu na marehemu Dk. Sengondo Mvungi.
Wengine ni Profesa Palamagamba Kabudi, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku na Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Yahya Msulwa.
Wengine ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Al-Shaymaa Kwegyir; Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (Tawla), Maria Kashonda; Mwantumu Malale, Esther Mkwizu, Humphrey Polepole, Jesca Mkuchu, John Nkolo, Riziki Mngwali, Richard Lyimo na mwanasheria maarufu, Said El- Maamry.
Kwa upande wa Zanzibar ni, Waziri Mkuu Mstaafu, Dk. Salim Ahmed Salim, Fatma Said Ali, Omar Sheha Mussa, Raya Salim Hamadi na mwanahabari Ally Saleh.
Wengine ni Awadh Ali Said, Ussi Khamis Haji, Salma Maoulidi, Nassor Khamis Mohammed, Simai Mohammed Said, Muhammed Yussuf Mshamba, Kibibi Mwinyi Hassan, Suleiman Omar Ali, Salama Kombo Ahmed na Abubakar Mohammed Ali.
Tume hiyo ilikuwa chini ya Katibu Assaa Ahmad Rashid na msaidizi wake, Casmir Sumba Kyuki ambaye ni Mwandishi Mkuu wa Sheria katika Wizara ya Katiba na Sheria.
Ilianza rasmi kazi ya kukusanya maoni ya wananchi Mei Mosi, mwaka juzi na baada ya kukamilisha kazi hiyo, iliyachambua na kuandika Rasimu ya Kwanza ya Katiba.
Kazi ya kukusanya maoni hayo iliwahusisha wananchi mmoja mmoja kupitia mikutano ya hadhara.
Baadaye Tume ilikutana na makundi maalumu na watu mashuhuri, wakiwamo viongozi wakuu wastaafu na waliopo madarakani, Januari 7-28, mwaka jana.
Baada ya kazi hiyo, Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal alizindua rasimu ya kwanza ya katiba Juni 4, mwaka jana.
Baadaye, mabaraza ya katiba ya wilaya ngazi ya kata yaliipitia rasimu hiyo kuanzia Julai 12 hadi Septemba 2, mwaka jana na kutoa mapendekezo yake ambayo yaliwasilishwa kwenye Tume hiyo.
Tume iliendelea kuyachambua mapendekezo ya mabaraza hayo ya katiba kabla ya kukabidhi rasimu ya pili kwa Rais Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein Desemba 30, mwaka jana.
KAULI YA JAJI WARIOBA
 Jaji Warioba jana baada ya taarifa ya Ikulu alijibu kwa kifupi kwamba: "Ni utaratibu wa kisheria, sheria ndivyo ilivyoelekeza."
Previous
Next Post »