BUNGE MAALUMU LA KATIBA SASA VULULU VULULU

bunge_72de4.jpg
Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Dodoma. Matarajio ya Bunge Maalumu la Katiba kukamilisha kanuni kwa maridhiano yaliyeyuka tena jana huku mambo ndani ya ukumbi yakionekana kuwa vululuvululu kwa baadhi ya wajumbe kuzungumza nje ya utaratibu na wengine kurushiana vijembe
.
Baadhi ya wajumbe waliamua kutoleana lugha chafu na kuweka kando hoja za msingi zinazowafanya watofautiane na kuchelewesha kazi ya kuandika Katiba Mpya.
Hali ilichafuka mchana wakati wajumbe walipokutana kupitisha kanuni baada ya mmoja wao, Felix Mkosamali kuomba mwongozo kwa Mwenyekiti wa muda, Pandu Ameir Kificho. Hata hivyo, Kificho alimtaka kukaa chini kwa muda kwa maelezo kuwa wajumbe waliofika katika kikao hicho walikuwa wachache, hivyo mwongozo wake kama ulikuwa unahitaji majibu ingekuwa vigumu kutolewa.
Baada ya muda alisimama, James Mbatia na kuomba mwongozo, akihoji sababu za kutaka kuanza kikao cha kupitisha kanuni hizo wakati wajumbe hawajapewa vitabu vya rasimu ya kanuni zenyewe.
"Mwenyekiti ulitangaza asubuhi kuwa tutagawiwa kanuni kabla ya saa tisa lakini hadi sasa tunataka kusomewa kanuni wakati hatujagawiwa kanuni hizo," alihoji Mbatia.
Kificho alitoa ufafanuzi kuwa kanuni hizo zilikuwa bado zinadurufiwa na kuwataka wajumbe wawe na nidhamu kwani anapotangaza wanapiga kelele.
Ghafla alisimama Mkosamali tena na kuwasha kipaza sauti na kuhoji kitendo cha mwenyekiti huyo kumpa Mbatia nafasi ya kutoa mwongozo wakati yeye amenyimwa... "Mwenyekiti hivi unaongozaje kikao, inakuwaje mimi nikuombe mwongozo uninyime na mwenzangu umpe? Mwenyekiti nakuheshimu sana, lakini sijui unatumia kanuni ipi kutoa nafasi kwa mjumbe wakati mimi ulinizuia nisiseme," alihoji Mkosamali.
Baada ya kauli hiyo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Hawa Ghasia aliwasha kipaza sauti na kwa sauti ya juu alisema "Mtoto mdogo hana adabu." Kauli hiyo iliibua hasira za Mjumbe mwingine, Moses Machali ambaye naye aliwasha kipaza sauti na kumjibu: "Kubwa jinga halina adabu," kauli iliyoibua miguno ndani ya Bunge.
Hata hivyo, licha ya Mwenyekiti kutoa onyo kwa kauli hizo kwamba hazifai, Mkosamali alisimama katika sehemu yake na kusema kuwa hakuna mtoto mdogo na kwamba tangu lini mtoto aliishinda CCM.
Chanzo cha tatizo
Chanzo cha mvurugano huo ambao wiki iliyopita kidogo usababishe ngumi kurushwa bungeni, ni mfumo wa upigaji kura katika kupitisha ibara za rasimu, ambao jana uliendelea kuwagawa wajumbe na kufanya ukumbi huo kuonekana kama eneo la mzaha.
Kauli za 'ndiyoooo', 'hapanaaaa' na vitendo vya kugonga meza viliongezeka katika kipindi cha asubuhi baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kuandaa Kanuni, Profesa Costa Mahalu kuwaleza wajumbe kuwa kamati yake haijafikia mwafaka wa ama iwe kura za siri au wazi na kwamba suala hilo limerejeshwa kwa wajumbe wenyewe
Profesa Mahalu alisema uamuzi unaachwa mikononi mwa Kamati ya Kudumu ya Bunge itakayoundwa baadaye. Alisema ili Bunge lisonge mbele baada ya kukwama kwa takribani wiki nzima, vifungu namba 37 na 38 vilivyozua utata vimerekebishwa.
"Tulizungumzia kanuni ya 37 na 38 zinazoelezea utaratibu kufanya uamuzi. Kanuni hizo sasa zitaeleza tu kwamba utaratibu wa uamuzi utakuwa ni wa kura, bila kusema ni ya siri ama ya wazi," alisema na kuongeza: "Lakini tumeona ni vizuri tukaweka fasili nyingine katika kifungu cha 38 ambayo itaeleza waziwazi kwamba ni aina gani ya kura itakayotumika na kwamba hiyo itategemea itakavyoamuliwa na Bunge hili.
Wajumbe wapinga
Mjumbe Profesa Ibrahim Lipumba ambaye pia ni Mwenyekiti wa CUF, alisema walichokubaliana katika Kamati ya Mashauriano ni kinyume na kilichoelezwa na Kamati ya Profesa Mahalu.
Alisema walikubaliana kuwa kifungu cha 37 na 38 visomeke kuwa mambo nyeti yaliyomo katika rasimu ya Katiba, yapigiwe kura ya siri na ya kawaida yapigiwe kura ya wazi.
"Tulichokubaliana ni tofauti kabisa na hiki ambacho kamati imekiwasilisha. Hatuwezi kufanya uamuzi wakati hatujafikia mwafaka," alisema Profesa Lipumba.
"Huku ni kukwepa uwajibikaji na haiwezekani tupitishe kanuni wakati baadhi ya vifungu havijakamilika. Kamati imepinga makubaliano yetu," alisema.
Mjumbe David Kafulila alisema: "Kwa namna tunavyokwenda, hakuna kinachoendelea, bado pande mbili zinavutana na kusababisha masuala yakwame. Tukikutana jioni (jana) na bado hali ni hii ya kupata taarifa nusunusu ambazo hazina mwafaka kuhusu jambo hili, tukubaliane kwamba semina hii isimame kwa muda, watu warudi majumbani kwao ili wafanye makubaliano huko nje."
Mwenyekiti Kificho alimjibu akisema Rais Kikwete ndiye aliyeitisha Bunge hilo na kwamba hata uamuzi wa kulivunja utafanywa na yeye.
Mjumbe Ezekiah Oluoch alisema iwapo Kamati ya Maridhiano iliyoanza kuketi Ijumaa imeshindwa kukubaliana, kilichopo sasa ni sekretarieti kuandaa karatasi za kura.
"Kwamba sisi tulikuchagua kwa kutumia kura ya siri, sasa tupige kura ya siri ambayo itaamua kura ambayo tunaitaka. Ikiwa tunakuja hapa jioni ukatuletea rasimu ya kanuni ambayo haina vifungu hivi 37 na 38 vya namna ya kufanya maamuzi, sidhani kama umetutendea haki kupitisha vitu nusu," alisema.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alijikuta katika wakati mgumu baada ya kuzomewa na baadhi ya wajumbe kwa madai ya kuwapotosha.
"Mimi nilivyoelewa wamesema tumepitisha vifungu 85 katika zile kanuni, vimebaki vifungu viwili 37 na 38 kwa uwiano wowote huwezi kusema kanuni imeshindwa," alisema Lukuvi na kuongeza:
"Tumeshaamua vifungu 85 na ili Kamati ya Kanuni ipate mamlaka ya kufanya marekebisho yoyote ya kanuni, lazima rasimu hii ipite kwanza."
Mchango wa Lukuvi ulionekana kuzidisha utata zaidi kwa wajumbe na hivyo Mwenyekiti Kificho kuwataka wajumbe wa Kamati ya Kanuni kufafanua zaidi.
Akitoa ufafanuzi kwa niaba ya wenzake, George Simbachawene ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alidai wajumbe hawakuwa wamemsikiliza vizuri Profesa Mahalu, kauli iliyozidisha mkanganyiko.
"Si kweli kwamba kanuni hizi zinapitishwa kasoro hivyo vifungu vya 37 na 38, bali vinapitishwa vyote isipokuwa kanuni hizo zitaishia tu kusema uamuzi utafanywa kwa kura basi.
"Hiyo siri mnayoitaka siyo hoja hapa... hoja hapa ni kupiga kura badala ya neno kura ya siri au ya wazi, tumesema utaratibu utakuwa ni wa kupiga kura," alisisitiza.
Alisema kamati yake imefikia hapo ili kuondoa dhana ya kwamba wanalipwa posho bure.
"Utaratibu wa kura gani itapigwa hauwezi kutupotezea muda hapa na kweli tuna uchungu na fedha za Watanzania, tunakula pesa bila kufanya kazi," alisema Simbachawene.
Nje ya Bunge
Mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale Mwiru alisema kinachofanyika ndani ya Bunge hilo sasa 'ni uhuni' ambao umemfanya awe kimya wakati wote na kushindwa kuzungumza.
Sipendi uhuni huo, ndiyo maana wakati wote nimekuwa kimya, lakini ukifika wakati wa kuijadili rasimu yenyewe nitazungumza kwa masilahi ya wananchi," alisema Kingunge.
Mjumbe Freeman Mbowe pamoja na kusema mvutano huo unatokana na kugawanyika kwa wajumbe wa Kamati ya Maridhiano, alipinga utaratibu uliopendekezwa kupitisha kanuni hizo nusunusu akisema ni mbovu kwa sababu vifungu wanavyotaka kuacha ndiyo nguzo ya mchakato wote wa Katiba.
"Huwezi kuweka sheria ya mchezo bila kuwa na sheria ya kufunga goli. Hapa tulipofikia lazima tupitishe sheria ya kupiga kura ndipo mambo mengine yafuate, kinyume chake hatufanyi kitu," alisema Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema.
Alisema ni afadhali taratibu nyingine zikasimama ili kusubiri kupitishwa kwa utaratibu wa kupiga kura badala ya kuendelea na mchakato huo ambao hatima yake iko shakani.
Alisema kura ya wazi ni hatari kwa kuwa itawagawa wananchi na wawakilishi wao bungeni.
Mjumbe mwingine, Yusuf Manyanga alisema: "Hapa bungeni tunayumbishwa na vyama vya siasa vyenye wabunge. Vimekuwa vikiweka masilahi ya vyama vyao mbele kuliko ya Watanzania."
Mjumbe mwingine Joseph Selasini alisema kilichoamuliwa na kamati hiyo siyo kulikabili tatizo, bali ni kuongeza ukubwa wa tatizo... "Hata jioni wajumbe watapingana tu na kamati, maana haiwezekani ukapitisha kanuni wakati vifungu havijakamilika."
Selasini alisema tatizo ni CCM kujiona kuwa ina mamlaka katika kila jambo na kusisitiza kuwa Tanzania siyo nchi ya chama hicho pekee.
Mjumbe Henry Shekifu alisema katika uandaaji wa kanuni, ikitokea kifungu kimoja kikaleta mvutano, lazima upitishaji wa kanuni hizo uendelee ili kuokoa muda, kauli ambayo iliungwa mkono na Mjumbe mwingine Martha Mlata.
Previous
Next Post »