WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amesema
kuwa serikali imeshindwa kuwapa wananchi maisha bora, licha ya nchi kuwa na
rasilimali nyingi.
Sitta ambaye pia ni spika wa
zamani wa Bunge, alisema kuna dalili za wazi za watu kukata tamaa, na kwamba
wako wachache wanajitajirisha, tena wengine kinyume cha katiba ya nchi na ile
ya CCM inayosema ‘sitakitumia cheo kwa faida yangu’.
Sitta alitoa kauli hiyo wakati
akihojiwa na kituo cha Star tv kwenye kipindi cha medani za kisiasa jana.
Alisema anasikitika kuona kuwa
hadi sasa Watanzania wana maisha magumu.
Pamoja na kutokitaja moja kwa
moja, ni wazi kuwa Sitta alikilenga Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwani ndicho
kinaongoza serikali aliyodai imeshindwa kuleta maisha bora yaliyoahidiwa kwa
wananchi.
“Tumepoteza hadhi ya nchi yetu,
ni aibu sana kusikia kuna vijana wa Kitanzania zaidi ya 600 waliopo katika
magereza mbalimbali duniani kwa sababu ya suala la dawa za kulevya.
“Inaumiza tunapoelekea 2015
kwenye uchaguzi mkuu tunawashabikia viongozi walioliingiza taifa letu katika
mikataba mibovu, zabuni za upendeleo na wengine bado wamewatumia vijana kama
punda kubeba dawa za kulevya,” alisema.
Alisisitiza kuwa katiba mpya
inayotengenezwa sasa ibane mianya hiyo.
Sitta aliongeza kuwa hali hiyo
ya matabaka ya matajiri na masikini ikizoeleka, taifa linaweza kuingia katika
machafuko makubwa.
Alisema hata mabilioni ya fedha
zilizopelekwa mikoani kwa ajili ya kuwainua wananchi, maarufu kama ‘mabilioni
ya Kikwete’ yametafunwa na wachache kwa kutumia miradi hewa.
“Tatizo hilo linaweza kumalizwa
na katiba mpya. Tukiwa na katiba mpya nzuri na viongozi waadilifu, sera za nchi
zitabadilika, Watanzania watapata maisha mazuri,” alisema.
Kuhusu uchaguzi mkuu ujao,
alitahadharisha kuwa kuna hatari kupitia uchaguzi huo Watanzania wakapata rais
aliyenunua uongozi kutokana na kusaidiwa kifedha na wafanyabiashara wasio
waadilifu.
Sitta aliweka bayana kuwa
uzalendo kwa viongozi nchini umeisha, na wale waliopo wanatanguliza ubinafsi
tofauti na ilivyokuwa enzi za Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Nyerere.
“Siku hizi baadhi ya viongozi
wa siasa wanajisifia kumiliki magari ya kifahari na nyumba za kisasa wakati
enzi za Mwalimu viongozi walikuwa wanaogopa hata kutaja kama wanamiliki nyumba
au gari.
“Ilikuwa si jambo la kawaida
watu kushabikia siasa za watu kununua wenzao, tofauti na ilivyo sasa. Watu
wanazoea utamaduni wa kusifia wenye fedha nyingi ingawa wapo katika utumishi wa
umma na hawasemi wamezipata wapi,” alisema.
Kuhusu suala la katiba mpya,
Sitta alisema itasaidia kuwa na upeo mpana wa demokrasia, na hivyo kuwataka
wananchi waondoe woga na kushiriki mchakato wake wa kuipata.
Sitta alisema upinzani nchini
unaendelea kupata nguvu na kuna vyama vinafanya vizuri, lakini akashauri kuwa
vingepata nguvu zaidi kama vingekuwa vichache.
“Upinzani utaimarika tukiweza
kushindana katika sera na mitazamo ya wapi tunaipeleka nchi. Tumeishakwenda
hatua fulani, lakini sasa inabidi hoja zitawale sio mabavu,” alisema.
Sitta aliongeza kuwa bado haoni
tishio lolote la upinzani kwa kuwa hawana safu kubwa ya orodha ya viongozi
wenye sifa za kugombea urais kama ilivyo kwa CCM, licha ya vyama hivyo kuwa na
watu wengi kwenye mikutano yao.
Kuhusu kambi za urais ndani ya
CCM, Sitta alisema zipo kwa kuwa wengine wanabebwa na wafanyabiashara, ingawa
hawana nia ya kuwasaidia wanyonge.
Kuhusu kujitosa katika mchakato
huo au la, alisema wakati bado na ukifika atapima wagombea ni akina nani na
kama naye atatamkwa tamkwa, uwezo wa kugombea anao.
Source:Tanzania Daima
EmoticonEmoticon