![images a3983](https://lh3.googleusercontent.com/blogger_img_proxy/AEn0k_tKaMBicrCc5e8t1Qqymy02OoBQGJa8k5urIN2YVoc83-pyUQfTXijQ_psiMHIJpPJYca-9guB6B5tgj_X4r4xTeic1F4QbmY0IlxYZjsrCNrER4gFP_p2org=s0-d)
Mamlaka
ya Chakula na Dawa (TFDA) ni taasisi iliyoundwa chini ya Sheria ya
Chakula Dawa na Vipodozi Sura ya 219, ili kudhibiti ubora na usalama wa
vyakula, dawa, vipodozi, na vifaa tiba kwa lengo la kulinda afya ya
jamii dhidi ya madhara yatokanayo na matumizi ya bidhaa hizo.
Imefahamika
kuwa mafuta yatokanayo na mimea hupendwa zaidi kuliko mafuta ya wanyama
kutokana na manufaa yake kiafya. Ili mafuta ya mimea yaweze kukidhi
vigezo vya ubora na usalama ni lazima yafanyiwe usafishaji (refining)
wakati wa usindikaji.
Hivi
karibuni kumekuwepo na ongezeko kubwa la matumizi ya bidhaa zinazotokana
na ubuyu ikiwa ni pamoja na mafuta yanayotokana na mbegu, unga wa mbegu
na majani ya mbuyu.
Taarifa za kisayansi zinaonesha kuwa mafuta ya ubuyu yana kiwango kikubwa cha tindikali ya mafuta aina ya cyclopropenoic
fatty acids ambayo huweza kusababisha athari ya kiafya endapo mafuta
hayo yatatumika kama chakula. Kiwango cha tindikali ya cyclopropenoic
fatty acids huweza tu kupunguzwa katika mafuta ya mbegu za ubuyu kwa
kuchemsha mafuta hayo katika nyuzi joto 180 kwa muda wa saa nane (8) au
kwa kutumia teknolojia ya kutengeneza mafuta mgando (hydrogenation). Kwa
sasa hapa nchini hakuna aina ya usindikaji unaofanyika wenye uwezo wa
kuondoa tindikali ya cyclopropenoic fatty acids katika mafuta ya mbegu
za ubuyu.
Baadhi ya
athari zinazoweza kutokana na matumizi ya mafuta ya ubuyu yenye
tindikali ya cyclopropenoic fatty acids ni pamoja na kuathiri
vimeng'enyo (enzymes) vinavyosaidia katika uchakataji wa tindikali za
mafuta mwilini (fatty acid biosynthesis
Aidha,
taarifa za kisayansi zinaonesha kuwa matumizi ya mafuta yenye kiasi
kikubwa cha cyclopropenoic fatty acids sanjari na matumizi ya vyakula
vilivyochafuliwa na sumu kuvu aina ya aflatoxin B1 ambayo inazalishwa na
ukungu (fungus) katika baadhi ya vyakula kama vile mahindi na karanga
huongeza uwezekano wa kuugua saratani.
Hadi sasa
hakuna kiwango chochote cha ubora na usalama cha kitaifa au kimataifa
cha mafuta yatokanayo na mbegu za ubuyu. Ili kuepuka athari zinazoweza
kujitokeza kutokana na matumizi ya mafuta ya mbegu za ubuyu, jamii
inashauriwa kuepuka ulaji wa mafuta hayo.
Hata
hivyo, tafiti za kisayansi hazijabainisha athari za kiafya zinazoweza
kutokana na ulaji wa bidhaa nyingine zitokanazo na ubuyu kama vile unga
wa ubuyu na majani ya mbuyu.
TFDA
inatoa wito kwa wananchi na jamii kwa ujumla kushirikiana katika jukumu
la kulinda afya za walaji kwa kutoa taarifa pale wanapouziwa au kuhisi
kuwepo kwa chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba duni na bandia ambavyo
havikidhi viwango vya usalama na ubora au pale sheria inapovunjwa ili
hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wahusika.
Kwa maelezo zaidi usisite kuwasiliana nasi kupitia;
Mkurugenzi Mkuu,
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA)
Barabara ya Mandela, Mabibo External,
S.L.P 77150
Dar Es Salaam, Tanzania
Simu: +255 22 2450512/2450751/2452108
Fax: +255 22 2450793
Tovuti: www.tfda.or.tz
EmoticonEmoticon