Lushoto. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wilayani Lushoto, mkoani Tanga, kimepata pigo baada ya Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kwekitui, Miraji Kassim kujiuzulu, kufuatia kile alichokielezea kuwa ni kukosa ushirikiano kutoka kwa viongozi wenzie ngazi ya kijiji ambao wote ni wa CCM.
Mwenyekiti huyo ambaye alichaguliwa Aprili 27 mwaka huu katika uchaguzi mdogo, aliwashangaza wafuasi wake baada ya Kaimu Mtendaji wa kijiji hicho Athumani Kibiriti, kusoma baraua ya kujiuzulu kwake katika mkutano wa hadhara.
Mkutano huo uliitishwa na Mbunge wa Bumbuli ambaye pia ni Naibu Waziri wa Sayansi na Teklonojia, January Makamba.
Akithibitisha hatua hiyo katika mkutano huo uliohudhiriwa na umati mkubwa wa watu, Mtendaji Kibiriti alisema mwenyekiti huyo amejiuzulu kwa ridhaa yake mwenyewe baada ya kukosa ushirikiano.
Alisema alipokea barua ya kujiuzulu kwa kiongozi huyo siku moja kabla ya mkutano huo na kwamba hakuwa amejua mwenyekiti wake ameandika ujumbe gani.
Alipotakiwa kueleza mahali alipo mwenyekiti huyo ili aweze kufungua mkutano huo, uliokuwa ukijadili maendeleo ya kijiji na wananchi kutoa kero zao, mtendaji alitoa barua ya mwenyekiti huyo kujiuzulu. Kitendo hicho kiliwafanya wafuasi wa Chadema kutoka ndani ya ukumbi wa mkutano wakiwa wanapiga kelele na kusema hawakubali kujiuzulu kwa mwenyekiti wao.
Mwananchi
EmoticonEmoticon