Simu ya mkononi iliyolowa maji.
Kuna wakati katika shughuli za kawaida inatokea kwa bahati mbaya simu ya mkononi inatumbukia kwenye maji na kulowa au hata kumwagikiwa na kimiminika cha aina yeyote labda chai, juisi, kahawa, soda nakadhalika lakini napenda kuzungumzia maji kama mfano mzuri.
Unaweza kujiepusha na hili lakini kwa kuwa kulowa hutokea kama ajali basi ikiwa simu yako ya mkononi imetumbukia kwenye maji na kulowa, fanya yafuatayo:
Hatua.
Zima simu yako baada ya kulowa au kutumbukia kwenye maji kama haikuzima yenyewe. Toa mfuniko wa betri na betri. Toa kadi ya simu, kisha kwa uangalifu toa mfuniko wa kicharazio na kicharazio (keypad).
Baada ya haya chukua kipande cha godoro ama kitambaa kisichotoa na kuacha nyuzinyuzi kwa urahisi na pangusa taratibu sehemu za simu yako ili kunyonya maji yaliyolowesha.
Ukimaliza zoezi hili unaweza kuanika sehemu za simu yako iliyolowa juani ama ukaziweka sehemu za simu yako juu ya mchele mkavu (ambao haujapikwa).
Mchele utafyonza unyevunyevu wote. Unaweza kufanya haya kwa muda wa dakika ishirini hivi.
Kisha kama utajiridhisha kwa kuona simu yako imekauka vizuri kabisa rudishia kila kitu cha kwenye simu yako vizuri ikiwemo betri, kicharazio (keypad) na kifuniko cha betri na jaribu kuwasha.
Kama simu yako haikupata hitilafu kubwa ilipolowa uwezekano wa simu yako kuwaka ni mkubwa lakini pia kama haitawaka ni vyema ukamuona fundi simu kwa matengezo zaidi
Laptop iliyolowa maji.
Wakati mwingine pia laptop inaweza kumwagikiwa na kimiminika chochote lakini napenda kuzungumzia maji kama mfano, maji yanapomwagikia kwenye laptop yako ni afadhali kuliko kimiminika kingine kinachonata kama soda, uji au juisi.
Kama tunavyojua maji ni mepesi na ni rahisi kitiririka kwa urahisi kuliko vimiminika vingine vizito vyenye kunata.
Kompyuta (laptop) yako inapomwagikiwa na maji sehemu zinazoathirika zaidi ni zile zenye upenyo wa kuwezesha maji kupenya kama keyboard, port za USB, HDMI nakadhalika. Unachotakiwa kufanya ni kama ifuatavyo.
HATUA.
1.
Kama baada ya laptop yako kumwagikiwa na maji haikuzima yenyewe basi izime.
2.
Chomoa vifaa vyovyote ulivyochomeka kwenye port za laptop.
-Ikishazima laptop toa betri, chomoa adapter cable kama ulikuwa ukichaji laptop na ondoa vifaa vyovyote ulivyochomeka kwenye port za laptop kama USB flash disk, external hard disk au external CD/DVD ROM.
Utafanya hivyo ili kuepusha shoti kwasabu maji yakishaingia kwenye vyanzo vya umeme husababisha shoti na hitilafu kubwa itakayoleta athari kwa vifaa vingine kwenye laptop.
3.
Igeuze laptop yako juu chini ili maji yaliloingia kwenye laptop yaweze kutiririka na kuepusha maji kuingia ndani zaidi kwenye mashine yako.
4.
Kausha sehemu yoyote unayoweza kukausha kwenye laptop yako kwa kutumia kitambaa laini kinachokausha vizuri bila kuacha nyuzinyuzi.
5.
Kama unaujuzi wa kutengeneza kompyuta, unaweza kuifungua laptop na kusambaratisha baadhi ya sehemu za laptop kama keyboard, cards na hard disk drive kisha futa kwa utaratibu na uhakikishe sehemu zote zilizoingiliwa na maji unazikausha bila kuacha unyevu unyevu.
Kama kuna uchavu au mnato wowote ufute ikiwezekana tumia brashi kama mswaki kusafisha ili kuepusha mgusano utakaosababisha shoti.
ANGALIZO:
Kama hauna ujuzi wowote wa kutengeneza komyuta (laptop) usithubutu kuifungua ni vyema ukapeleka kwa fundi au kumpa mtu mwenye ujuzi akusaidie.
Unashauriwa baada ya kufuta laptop yako vizuri acha kwa muda wa saa 24 mpaka saa 48 ili uwe na uhakika imekauka vizuri kabisa.
Kama laptop yako ilimwagikiwa na maji kidogo basi heri zaidi angalau iache kwa saa 12 kisha rudishia vifaa vyote ulivyosambaratisha kwa kuvifunga vizuri na jaribu kuwasha.
Kama laptop yako haitawaka basi ipeleke kwa fundi wa kompyuta kwa matengenezo zaidi.
Kama una chochote cha kuongeza kuhusiana na mada hapo juu, tafadhali usisite kutoa maoni yako
EmoticonEmoticon